As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakatuh! Uislamu ni dini ya amani, rehema na haki. Tofauti za kifiqhi na kimtazamo (madhehebu) zimekuwepo tangu zama za Maswahaba,tangu zama za Maswahaba wa Mtume (S.A.W.), lakini hazikuwa chanzo cha uhasama wala migawanyiko. Qur’ani Tukufu inaelekeza Waumini kuishi kwa amani, kuheshimiana na kushikamana, licha ya tofauti zilizopo. Kuishi kwa amani na madhehebu mengine ni msingi wa kulinda umoja wa Umma na heshima ya Uislamu.
Qur’ani tukufu Inahimiza Umoja na Kukataza Migawanyiko, Mwenyezi Mungu anasema: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote kwa pamoja, wala msifarakane.”Suratu Aal ‘Imraan 3:103. Aya hii inaweka wazi kuwa migawanyiko ya madhehebu haipaswi kuvunja mshikamano wa Waislamu.
Pia, Qur’ani tukufu inatambua kuwepo kwa tofauti miongoni mwa watu: “Lau Mola wako angelipenda, angewafanya watu wote umma mmoja.”Suratu Hud 11:118. Hii inaonesha kuwa tofauti za mitazamo ni sehemu ya mpango wa Mwenyezi Mungu, na si sababu ya chuki.
Hata hivyo Qur’ani tukufu inakataza chuki na uadui, Mwenyezi Mungu anawaonya Waumini: “Wala chuki ya watu isikuchocheeni mkose kuwa waadilifu.”Suratul Maa’idah 5:8. Hata katika tofauti za madhehebu, uadilifu na heshima vinapaswa kutangulizwa.
Kuishi kwa amani ni sehemu ya maadili ya kiislamu, Qur’ani inawahimiza Waumini kutumia maneno na njia bora: “Waambieni watu maneno mazuri.”Suratul Baqarah 2:83, “Na semeni yaliyo bora.”Suratul Israa 17:53. Maneno mazuri hujenga amani na huondoa migogoro.
Pia, Qur’ani tukufu inakataza kulazimisha Imani Mwenyezi Mungu anasema: “Hakuna kulazimisha katika dini.”Suratul Baqarah 2:256. Aya hii ni msingi wa kuheshimu tofauti za kimtazamo na kimadhehebu. Mtume (S.A.W.) hakulazimisha watu kukubali mitazamo fulani ya kifiqhi, bali aliheshimu tofauti zenye dalili.
Kufuata njia ya hekima na mawaidha mema, Qur’ani inatoa mwongozo wa namna ya kushughulikia tofauti: “Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema.”Suratun-Nahl 16:125. Hekima na busara huzuia migongano ya kimadhehebu.
Qur’ani inatahadharisha: “Wala msizozane, mkashindwa nguvu zenu zikapotea.”Suratul Anfaal 8:46. Migogoro ya madhehebu huondoa nguvu, heshima na maendeleo ya Waislamu.
Waumini ni Ndugu, Qur’ani tukufu inasisitiza udugu wa Kiislamu: “Hakika Waumini ni ndugu.”Suratul Hujuraat 49:10. Udugu huu haupaswi kuvunjwa na tofauti za madhehebu.
Ndugu zangu waislamu Mwenyezi Mungu anapenda wapatanishi. Tukirejea katika Qur’ani tukufu inawahimiza Waumini kuwa wapatanishi: “Basi suluhisheni baina ya ndugu zenu.”Suratul Hujuraat 49:10. Kuishi kwa amani na madhehebu mengine ni ibada inayopendwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, kuishi kwa amani na madhehebu mengine si hiari bali ni wajibu wa Kiislamu. Uislamu unahimiza kuheshimu tofauti za kifiqhi na kimtazamo, kudumisha umoja wa Waumini, kutumia hekima, upole na maneno mazuri na kuepuka chuki na migawanyiko.
Kwa kuzingatia mwongozo huu wa Qur’ani, Waislamu wataendelea kuwa Umma mmoja wenye amani, nguvu na heshima, licha ya tofauti zilizopo.
0 Comments