Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni msimu wa rehema, msamaha na malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Miongoni mwa amali zenye thawabu kubwa katika mwezi huu ni kumfuturisha aliyefunga. Kitendo hiki kinaonesha upendo, mshikamano na huruma miongoni mwa Waumini, na kimeahidiwa malipo makubwa katika Qur’aan na Sunnah.
Kumfuturisha Ni Katika Wema na Ihsani. Mwenyezi Mungu anasema: “Na fanyeni wema; hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao wema.” (Surat Al-Baqarah 2:195)
Kumfuturisha aliyefunga ni katika wema (ihsani) ambao Allah anaupenda. Ni sadaka na ni msaada kwa ndugu yako katika ibada.
Aidha, Allah (S.W.T) anasema: “Na wanawalisha chakula, kwa kupenda Kwake, masikini, yatima na mateka. (Wakisema): Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu; hatutaki kwenu malipo wala shukrani.”(Surat Al-Insan 76:8–9)
Aya hizi zinaonesha daraja ya juu ya kulisha wengine kwa ajili ya Allah pekee.
Hupata Thawabu Sawa na Aliyefunga, Mtume Muhammad (S.A.W) amesema: “Atakayemfuturisha aliyefunga, atapata thawabu kama zake bila kupungua chochote katika thawabu za aliyefunga.” (Imepokewa na At-Tirmidhi – Hadithi Sahihi)
Hii ni bishara kubwa sana. Unaweza kupata malipo ya saumu kwa kumfuturisha tu ndugu yako, hata kwa tende chache au maji.
Njia ya Kuokoka na Moto, Ramadhani ni mwezi wa kuokolewa na Moto. Mtume (S.A.W) amesema: “Jiepusheni na Moto hata kwa kutoa sadaka ya kipande cha tende.” (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim)
Ikiwa kipande cha tende kinaweza kuwa kinga ya Moto, basi kumfuturisha aliyefunga — hasa mwenye uhitaji — ni sababu kubwa ya kupata rehema na kuokoka na adhabu.
Mfano wa Mtume (S.A.W) Katika Ukarimu, Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas (R.A): “Mtume (S.A.W) alikuwa mkarimu zaidi kuliko watu wote, na alikuwa mkarimu zaidi katika Ramadhani…” (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim)
Hii inaonesha kuwa Ramadhani ni mwezi wa kuongeza ukarimu na kuwajali wengine.
Baraka ya Dua ya Mfungaji, Mtume (S.A.W) amesema: “Hakika mfungaji ana dua isiyokataliwa wakati wa kufuturu kwake.” (Imepokewa na Ibn Majah – Hadithi Hasan)
Fikiria baraka ya kumfuturisha mtu, kisha akakuombea dua njema wakati wake wa kufuturu! Hiyo ni fursa ya kupata dua yenye kukubaliwa.
Kumfuturisha katika mwezi wa Ramadhani ni amali nyepesi lakini yenye thawabu kubwa sana. Ni njia ya Kupata malipo sawa na mfungaji, Kujipatia mapenzi ya Allah, Kuongeza mshikamano wa Kiislamu, Kuokoka na Moto naKupata dua za baraka
Tusisubiri kuwa matajiri ili tufanye hili. Hata tende moja au glasi ya maji vinaweza kuwa sababu ya kuandikiwa thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Tuombe Allah (S.W.T) atufanye tuwe miongoni mwa wanaowalisha na kuwafuturisha Waumini kwa ajili Yake, na atuandikie thawabu kubwa katika mwezi huu mtukufu.
Allahumma taqabbal minna wa ja’alnaa minal-muhsiniin. Aamiin.
0 Comments