Mwezi wa Ramadhani ni mgeni mtukufu anayekuja na rehema, maghfira na kuokolewa na Moto wa Jahannam. Si kila anayetamani Ramadhani huufikia, wala si kila anayefikia huweza kuutumia ipasavyo. Kwa sababu hiyo, Uislamu unatufundisha kujiandaa mapema kiibada, kimoyo na kivitendo ili tuupokee Ramadhani kwa imani, ikhlasi na bidii.
Ramadhani ni mwezi wa ibada maalumu, Mwenyezi Mungu anasema: “Mwezi wa Ramadhani ni mwezi ulioteremshwa Qur’ani, uwe ni uongofu kwa watu na dalili zilizo wazi za uongofu na upambanuzi.”Suratul-Baqarah 2:185
Aya hii inaonesha kuwa Ramadhani ni mwezi wa Qur’ani, mwezi wa uongofu na mwezi wa mabadiliko ya kiroho. Hivyo, maandalizi ya Ramadhani ni jambo la lazima kwa Muumini makini.
Kujiandaa kwa toba na kusafisha moyo, Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Tubieni kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli.” Suratut-Tahriim 66:8.
Kujiandaa Ramadhani kunaanza kwa kutubu madhambi, kuacha maovu, kusameheana na kurekebisha mahusiano. Mtume Muhammad (S.A.W.) amesema: “Mwenye kutubu kutokana na dhambi ni kama asiye na dhambi.”Hadithi Hasan: Ibn Maajah
Kujiandaa kwa Kuongeza Ibada za Sunnah, Mtume (S.A.W.) alikuwa akijiandaa Ramadhani kwa vitendo. Bi ‘Aishah (R.A.) amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akifunga sana katika mwezi wa Sha‘aban.”Sahih Al-Bukhari na Muslim. Hii ni dalili kuwa Saumu za Sunnah, Swala za Sunnah na dhikri ni maandalizi muhimu kabla ya Ramadhani.
Kujiandaa kwa Kusoma na Kuitafakari Qur’ani, Mwenyezi Mungu anasema: “Na hii ni Qur’ani Tuliyoiteremsha ikiwa imebarikiwa, basi ifuateni.”Suratul-An‘aam 6:155. Ramadhani ni mwezi wa Qur’ani, hivyo kupanga ratiba ya kusoma Qur’ani, kujifunza tafsiri na kuizoesha nafsi na Qur’ani ni maandalizi ya lazima.
Kujiandaa kwa Dua na Unyenyekevu, Mwenyezi Mungu anasema: “Na Mola wenu amesema: Niombeni, Nitakujibuni.”Suratu Ghaafir 40:60
Mtume (S.A.W.) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkarimu, hupenda aombwapo.”Hadithi Sahihi: At-Tirmidhiy. Kujiandaa Ramadhani kunahusisha kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie uhai na afya, ikhlasi katika ibada na kukubaliwa kwa matendo.
Kujiandaa kwa Nidhamu ya Maisha Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi hali ya watu mpaka wabadilishe yaliyo ndani ya nafsi zao.”Suratur-Ra‘d 13:11. Ramadhani unahitaji kupanga muda wa ibada, kupunguza mambo yasiyo ya lazima, kudhibiti ulimi, macho na masikio.
Mtume (S.A.W.) amesema: “Yeyote asiyeyaacha maneno ya uongo na kuyatenda, Mwenyezi Mungu hana haja na kuacha kwake kula na kunywa.”Sahih Al-Bukhari
Kujiandaa kwa Sadaka na Msaada, Mtume Muhammad (S.A.W.) alikuwa mkarimu sana, hasa Ramadhani: “Mtume alikuwa mkarimu zaidi, na alikuwa mkarimu zaidi katika Ramadhani.”Sahih Al-Bukhari na Muslim
Hivyo, maandalizi ya Ramadhani yahusishe kusaidia maskini, kuwafariji wenye shida na kuzoea kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Kujiandaa kwa Nia ya Mabadiliko, Mwenyezi Mungu anasema: “Na Mwabuduni Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi.”Suratul-Bayyinah 98:5. Ramadhani si mwezi wa njaa tu, bali ni mwezi wa mabadiliko ya tabia, mwezi wa kujenga uchaMungu na mwanzo wa maisha mapya ya utiifu.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W.), kujiandaa kiibada kwa Ramadhani ni dalili ya imani iliyo hai, sababu ya kunufaika na fadhila za Ramadhani na njia ya kupata msamaha na radhi za Mwenyezi Mungu.
Hivyo, tujianze leo kujiandaa kwa toba, dua, Qur’ani, Saumu za Sunnah na matendo mema, ili Ramadhani itufikie tukiwa tayari kimoyo na kivitendo.
Dua ya Maandalizi “Ewe Mwenyezi Mungu, tufikishe Ramadhani, tujaalie kuifunga na kuisimamia kwa imani na ikhlasi, na ukubali ibada zetu.” Aamiyn.
0 Comments