Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wenye daraja kubwa na utukufu wa kipekee mbele ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala). Ni mwezi wa rehema, maghfira (msamaha) na kuokolewa na Moto. Ndani yake zipo fadhila nyingi zilizoelezwa katika Qur’aan Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W).
Ramadhani Ni Mwezi wa Kushushiwa Qur’aan, Mwenyezi Mungu anasema:
“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani, iwe ni uwongofu kwa watu na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi…” (Surat Al-Baqarah 2:185)
Aya hii inaonesha wazi kuwa Ramadhani umepewa heshima kubwa kwa sababu ni mwezi ambao Qur’aan ilianza kushushwa. Hivyo, ni mwezi wa kuisoma, kuitafakari na kuifuata Qur’aan katika maisha yetu.
Kufunguliwa Milango ya Peponi na Kufungwa Milango ya Motoni, Mtume Muhammad (S.A.W) amesema: “Inapoingia Ramadhani, milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa, na mashetani hufungwa minyororo.” (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim)
Hii ni bishara kubwa kwa Waumini. Inaonesha kuwa Ramadhani ni fursa adhimu ya kuongeza ibada na kuacha maasi.
Kusamehewa Madhambi, Mtume (S.A.W) amesema: “Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kutaraji malipo kwa Mwenyezi Mungu, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.” (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim)
Fadhila hii ni zawadi kubwa sana. Ramadhani ni mwezi wa kutubia kwa dhati na kurejea kwa Allah.
Usiku wa Lailatul-Qadr, Katika Ramadhani upo usiku wenye thamani kuliko miezi elfu moja. Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Sisi tumeiteremsha (Qur’aan) katika Usiku wa Cheo. Na nini kitakachokujulisha nini Usiku wa Cheo? Usiku wa Cheo ni bora kuliko miezi elfu moja.” (Surat Al-Qadr 97:1–3)
Ibada ya usiku huu ni bora kuliko ibada ya miaka zaidi ya themanini. Huu ni mwezi wa kutafuta Lailatul-Qadr kwa kuswali, kuomba dua na kufanya dhikri nyingi.
Ramadhani Ni Mwezi wa Taqwa, Allah (S.W.T) anasema: “Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa saumu kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu (Taqwa).” (Surat Al-Baqarah 2:183)
Lengo la saumu si njaa tu, bali ni kujenga uchamungu, nidhamu, subira na utii kwa Mwenyezi Mungu.
Dua Hukubaliwa, Mtume (S.A.W) amesema: “Watu watatu dua yao haikataliwi: Mfungaji mpaka afuturu, kiongozi mwadilifu, na aliyedhulumiwa.” (Imepokewa na At-Tirmidhi – Hadithi Hasan)
Hivyo Ramadhani ni wakati wa kuomba dua kwa wingi – kujiombea nafsi zetu, familia zetu na Ummah mzima.
Ramadhani Ni Mwezi wa Sadaka na Ukarimu, Mtume (S.A.W) alikuwa mkarimu zaidi katika Ramadhani kuliko wakati mwingine wowote. Ibn Abbas (R.A) amesema kuwa Mtume alikuwa mkarimu sana, na ukarimu wake uliongezeka zaidi katika mwezi wa Ramadhani. (Imepokewa na Al-Bukhari)
Hii inatufundisha kuongeza sadaka, kuwasaidia wahitaji na kufuturisha waliofunga. Ramadhani ni zawadi adhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni mwezi wa Qur’aan, Saumu, Toba, Dua, Sadaka, Kusamehewa madhambi.
Ni wajibu wetu kuuthamini, kujiandaa nao kwa ibada, na kuutumia kama fursa ya kubadilisha maisha yetu. Tuombe Mwenyezi Mungu atujalie tuufikie Ramadhani, atupe nguvu za kuutumikia kwa ibada na atuandikie katika waliokombolewa na Moto.
Allahumma ballighnaa Ramadhani, wa a’innaa ‘alaa siyaamihi wa qiyaamihi, wa taqabbal minna. Aamiin.
0 Comments