As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakatuh!. Mwislamu mwenzangu naomba utambue kuwaUislamu si dini ya ibada za kimwili pekee, bali ni dini inayojenga moyo, tabia na mwenendo wa maisha ya Muislamu. Miongoni mwa amali zilizopewa uzito mkubwa katika Qur’ani Tukufu ni tabia njema (Akhlaq).
Mwenyezi Mungu anawapima Waumini si kwa ibada zao tu, bali pia kwa namna wanavyotendeana na wanadamu wenzao. Tabia njema ni alama ya imani ya kweli na njia ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Qur’ani tukufu inafungamanisha imani na matendo mema, ambayo msingi wake ni tabia njema: “Hakika wale walioamini na wakatenda mema, watapata Pepo.”Suratul Kahf 18:107. Matendo mema hayawezi kutenganishwa na tabia njema kama uaminifu, subira, unyenyekevu na huruma.
Pia, Mtume Muhammad (S.A.W.) akasema:Waumini waliokamilika zaidi katika imani ni wale wenye tabia njema zaidi.”Hadithi Sahihi: Imepokewa na At-Tirmidhiy. Hii inaonesha kuwa ukamilifu wa imani hupimwa kwa tabia, si maneno peke yake.
Ukimwangalia Mtume Muhammad (S.A.W.) ni Mfano wa Tabia Njema. Mwenyezi Mungu anamuelezea Mtume wake kwa sifa adhimu ya tabia njema: “Na hakika wewe una tabia tukufu kabisa.”Suratul Qalam 68:4. Aya hii inaonesha kuwa tabia njema ni kilele cha ukamilifu wa mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Haya hivyo, Qur’ani tukufu imeweka misingi ya tabia njema katika jamii: “Hakika Mwenyezi Mungu huamrisha uadilifu, ihsani, na kuwapa jamaa; na hukataza uchafu, uovu na dhulma.”Suratun-Nahl 16:90. Aya hii ni muhtasari wa maadili yote mema anayoyapenda Mwenyezi Mungu.
Pia, Qur’ani inawahimiza Waumini kuishi kwa upole na maneno mazuri: “Waambieni watu maneno mazuri.”Suratul Baqarah 2:83, “Na semeni yaliyo bora.”Suratul Israa 17:53. Maneno mazuri ni msingi wa amani, mshikamano na heshima katika jamii.
Ewe mwislamu mwezangu tambua kuwa Subira na Msamaha ni Tabia Anazozipenda Allah. Mwenyezi Mungu anawapenda wenye subira na msamaha: “Na wanaokandamiza hasira zao na kuwasamehe watu; na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.”Suratu Aal ‘Imraan 3:134. Aya hii inaonesha wazi kuwa kudhibiti hasira na kusamehe ni miongoni mwa amali bora.
Qur’ani tukufu inawakataza Waumini kuwa na tabia mbaya: “Wala usiwadharau watu, wala usitembee katika ardhi kwa majivuno.”Suratu Luqmaan 31:18. Tabia njema huambatana na unyenyekevu na heshima kwa wengine.
Mwenyezi Mungu anaahidi daraja ya juu kwa wenye tabia njema: “Hao watapewa malipo mara mbili kwa sababu ya subira yao.”Suratul Qasas 28:54. Hii ni dalili kuwa tabia njema ina thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Qur’ani inafundisha kulipiza uovu kwa wema: “Lipa uovu kwa lililo bora; ndipo yule uliye na uadui naye atakuwa kama rafiki wa karibu.”Suratul Fussilat 41:34. Hii ni ngazi ya juu ya tabia njema inayobadilisha chuki kuwa upendo.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, tabia njema ni miongoni mwa amali bora zaidi anazozipenda Mwenyezi Mungu. Imani ya kweli huonekana kupitia uadilifu, subira na msamaha, maneno na matendo mema, unyenyekevu na heshima kwa wengine.
Muislamu anapaswa kutambua kuwa ibada zake zitakuwa na uzito mkubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu endapo zitakwenda sambamba na tabia njema. Kwa kufanya hivyo, tutapata radhi za Mwenyezi Mungu, amani katika jamii na mafanikio ya dunia na Akhera.
0 Comments