MISIMAMO MIKALI YA KIITIKADI, CHANZO CHA KUTUGAWA WAISLAMU
Na Haseeb S Izaan
As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakatuh! Uislamu ni dini ya wastani, rehema na umoja. Hata hivyo, misimamo mikali ya kiitikadi ambayo hujikita katika kupitiliza mipaka, kuhukumu wengine kwa ukali, na kujiona wenye haki pekee imekuwa chanzo cha migawanyiko mikubwa miongoni mwa Waislamu. QUR’ANI Tukufu na MTUME MUHAMMAD (S.A.W.) wameonya vikali dhidi ya hali hii, na wakahimiza hekima, uadilifu na mshikamano.
Qur’ani na Sunnah zinakataza imani ya kupindukia katika Dini, Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msipite mipaka katika dini yenu.”Suratun-Nisaa 4:171. Aya hii inabainisha kuwa kupindukia iwe kwa kauli, hukumu au vitendo ni kinyume na misingi ya Uislamu.
Pia, Mtume Muhammad (S.A.W.) akasisitiza hilo hilo: “Epukeni kupindukia katika dini, kwani waliangamizwa waliokuwa kabla yenu kwa sababu ya kupindukia katika dini.”Hadithi Sahihi: Imepokewa na An-Nasaai na Ibn Maajah. Hii inaonesha wazi kuwa misimamo mikali si njia ya uongofu bali ni sababu ya maangamizi.
Uislamu unahimiza umoja na kuzuia mifarakano ya kiitikadi: Qur’ani inawaamrisha Waumini: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote kwa pamoja, wala msifarakane.”Suratu Aal ‘Imraan 3:103. Misimamo mikali huwafanya Waislamu kujiona wao pekee ndio sahihi, na wengine kuwatenga—hali inayovunja amri hii ya Qur’ani.
Mtume (S.A.W.) akasema alisisitiza pia: “Muumini kwa Muumini mwenzake ni kama jengo; sehemu moja huimarisha nyingine.”Sahih Al-Bukhari na Sahih Muslim. Misimamo mikali hubomoa “jengo” hili la udugu na mshikamano.
Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika wale walioigawanya dini yao na wakawa makundi, huna uhusiano nao wowote.”Suratul An‘aam 6:159. Aya hii inaonya dhidi ya itikadi finyu zinazojenga uhasama badala ya udugu.
Mtume (S.A.W.) akatahadharisha: “Hakika umma wangu utagawanyika… na wokovu utakuwa kwa wale wanaofuata niliyo juu yake mimi na Maswahaba wangu.”Hadithi Hasan: At-Tirmidhiy. Hii inaonesha kuwa njia sahihi ni kufuata Qur’ani na Sunnah kwa uelewa wa Maswahaba, si misimamo mikali ya kikundi.
Misimamo mikali huzaa chuki na hukumu za haraka, Qur’ani inasema: “Wala chuki ya watu isikuchocheeni mkose kuwa waadilifu.”Suratul Maa’idah 5:8. Misimamo mikali mara nyingi husababisha kuhukumu wengine kwa ukali, jambo linalokiuka haki na uadilifu.
Mtume (S.A.W.) alisema; “Tahadharini na dhulma, kwani dhulma ni giza Siku ya Kiyama.”Sahih Muslim. Misimamo mikali huwafanya baadhi ya watu kuwahukumu wengine bila haki, jambo linalopingana na maadili ya Kiislamu.
Uislamu ni dini ya wastani, Mwenyezi Mungu anasema: “Na kadhalika tumekufanyeni umma wa wastani.”Suratul Baqarah 2:143. Wastani huu unapingana moja kwa moja na itikadi kali zinazotaka kupitiliza au kulazimisha mitazamo.
Mtume (S.A.W.) akasema: “Hakika dini hii ni nyepesi, wala hakuna anayejikaza katika dini ila atashindwa.”Sahih Al-Bukhari. Uislamu hauhimizi misimamo mikali, bali urahisi na uwiano.
Qur’ani inasema: “Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema.”Suratun-Nahl 16:125. Hivyo, kulazimisha mtazamo mmoja kwa ukali ni kupinga hikima ya Mwenyezi Mungu.
Mtume (S.A.W.) akasema: “Upole hauwepo katika jambo lolote ila hulipamba, na hauondolewi katika jambo lolote ila huliharibu.”Sahih Muslim. Misimamo mikali hukosa upole, hivyo huharibu badala ya kujenga.
Qur’ani inatahadharisha: “Wala msizozane, mkashindwa nguvu zenu zikapotea.”Suratul Anfaal 8:46. Hii ni tahadhari kuwa misimamo mikali huondoa nguvu, heshima na umoja wa Umma.
Mtume (S.A.W.) akasema: “Muumin ni ndugu wa Muumin mwenzake; hamdhulumu wala humsaliti.”Sahih Muslim. Misimamo mikali huvunja udugu na kuondoa nguvu ya pamoja ya Umma.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W.), misimamo mikali ya kiitikadi si katika mafundisho ya Uislamu, husababisha migawanyiko, chuki na udhaifu, na huondoa rehema na hekima ya dini. Kwa kufanya hivyo, Umma wa Kiislamu utaendelea kuwa umoja mmoja wenye amani, nguvu na heshima.
0 Comments