FADHILA NA SIFA KUU ZA SIKU YA IJUMAA KWA MUJIBU WA QUR’ANI TUKUFU
Na Haseeb S Izaan
As-salāmu ‘alaykum wa raḥmatullāhi wa barakātuh! Siku ya Ijumaa ni siku tukufu na bora zaidi katika siku za wiki kwa Waislamu. Mwenyezi Mungu ameipa siku hii heshima ya pekee na akaifanya kuwa siku ya ibada ya pamoja, kukumbushana, kuimarisha umoja na kuhuisha imani. Qur’ani Tukufu imeitaja siku ya Ijumaa kwa jina lake, jambo linaloonesha hadhi yake ya juu katika Uislamu.
Mwenyezi Mungu ametaja siku hii katika Qur’ani Tukufu kwa heshima kubwa: “Enyi mlioamini! Inapoitwa Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na acheni biashara.”Suratul Jumu‘ah 62:9. Kutajwa kwa siku hii moja kwa moja ni dalili ya nafasi yake ya kipekee mbele ya Mwenyezi Mungu.
Ijumaa ni Siku ya Dhikri na Kumbukumbu ya Mwenyezi Mungu, Qur’ani inaelekeza Waislamu kuipa kipaumbele dhikri siku ya Ijumaa: “…nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu…”Suratul Jumu‘ah 62:9. Dhikri hii inajumuisha Swala ya Ijumaa, khutba, kusikiliza mawaidha na kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu.
Aidha, Ijumaa ni Siku ya Umoja wa Waumini, Swala ya Ijumaa hukusanya Waislamu pamoja bila ubaguzi wa rangi, cheo au kabila: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote kwa pamoja, wala msifarakane.”Suratu Aal ‘Imraan 3:103. Ijumaa huimarisha udugu, mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu.
Ijumaa Inatanguliza Ibada Kuliko Maslahi ya Dunia, Qur’ani inawahimiza Waumini kuacha shughuli za dunia kwa ajili ya ibada: “Na acheni biashara; hayo ni bora kwenu ikiwa mnajua.”Suratul Jumu‘ah 62:9. Hii ni fadhila kubwa inayomfundisha Muislamu kuweka mizani sahihi kati ya dunia na Akhera.
Qur’ani inawahimiza waisamu wote kuwa, Baada ya Swala, Ruhusa ya Kutafuta Riziki Halali. Uislamu haukati kazi, bali huipanga kwa mizani sahihi: “Na itakapo kwisha Swala, tawanyikeni katika ardhi na tafuteni fadhila za Mwenyezi Mungu.”Suratul Jumu‘ah 62:10. Aya hii inaonesha kuwa Ijumaa ni mfumo kamili wa maisha—ibada na kazi kwa uwiano.
Ijumaa ni Siku ya Kumbusho na Mafunzo ya Dini, Khutba ya Ijumaa ni chombo cha kuelimisha na kukumbusha: “Basi kumbusha; kwani kukumbusha kunawafaa Waumini.”Suratudh-Dhaariyaat 51:55. Kila Ijumaa ni fursa ya kujirekebisha, kutubu na kuimarisha imani.
Kuitikia wito wa Swala ya Ijumaa ni ishara ya Imani, Ijumaa ni Alama ya Uchamungu na Utii: “Hayo ni bora kwenu ikiwa mnajua.”Suratul Jumu‘ah 62:9. Kuhudhuria Swala ya Ijumaa huongeza daraja la uchamungu na utii kwa Mwenyezi Mungu.
Kupitia mawaidha ya mara kwa mara, jamii huimarika kimaadili:
“Hakika Mwenyezi Mungu huamrisha uadilifu na ihsani.”Suratun-Nahl 16:90. Khutba za Ijumaa huwa chachu ya uadilifu, amani na maadili mema.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, siku ya Ijumaa ni siku yenye fadhila na heshima ya kipekee, iliyowekwa kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa pamoja, kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu, kusikiliza mawaidha na kujirekebisha, na kuweka mizani sahihi kati ya dunia na Akhera.
Ni wajibu wa kila Muislamu kuitukuza siku ya Ijumaa kwa kuhudhuria Swala yake, kusikiliza mawaidha, na kuijaza siku hii kwa dhikri na matendo mema ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
0 Comments