HII NDIYO AQIYDAH (ITIKADI) SAHIHI YA KIISLAMU KWA MUJIBU WA QUR’ANI TUKUFU
Na Haseeb S Izaan
As-salāmu ‘alaykum wa raḥmatullāhi wa barakātuh! Aqiydah (Itikadi) ya Kiislamu ni msingi mkuu wa dini ya Uislamu. Ni imani thabiti inayojengwa juu ya Qur’ani Tukufu na inamwelekeza Muislamu katika kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa usahihi, kufuata Mtume Muhammad (S.A.W.), na kuishi maisha yenye maadili mema. Aqiydah sahihi humlinda Muislamu dhidi ya upotovu, imani potofu na misimamo mikali. Qur’ani Tukufu imeweka wazi vipengele vya itikadi sahihi ili kila Muislamu awe na mwongozo wa kweli.
Msingi mkuu wa Aqiydah ya Kiislamu ni Tauhidi, kumuamini Mwenyezi Mungu mmoja bila mshirika. Qur’ani Tukufu inatufafanulia kuwa; “Na Mola wenu ni Mungu Mmoja tu; hapana mungu isipokuwa Yeye, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”Suratul Baqarah 2:163.
Pia inaendela kueleza; “Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni Mmoja.”Suratul Ikhlaas 112:1. Tauhidi humuweka Muislamu mbali na shirki, ushirikina na kuabudu chochote kisichokuwa Mwenyezi Mungu.
Aqiydah sahihi inahusisha kumuamini Mwenyezi Mungu kwa Majina na Sifa Zake kama zilivyokuja katika Qur’ani bila kupotosha wala kufananisha: “Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri; basi mwombeni kwa majina hayo.” Suratul A‘raaf 7:180.
“Hapana chochote kinachofanana na Yeye, naye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”Suratush-Shuuraa 42:11.
Ndugu msomaji nadhani sote tunafahamu kuwa Malaika ni viumbe wa Mwenyezi Mungu wanaotekeleza amri Zake, katika Qur’ani Tukufu imeelezea kuwa;“Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waumini pia; wote wanamuamini Mwenyezi Mungu, Malaika Wake…”Suratul Baqarah 2:285.
Qur’ani Tukufu inatusihi Kumuamini Vitabu vya Mwenyezi Mungu. Aqiydah sahihi inajumuisha kuamini vitabu vyote vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, huku Qur’ani ikiwa ya mwisho na kamilifu: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa haki, na kwa haki imeteremshwa.”Suratul Israa 17:105.
Pia, Uislamu unawaheshimu Mitume wote bila kuwabagua: “Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume Wake.”Suratul Baqarah 2:285.
“Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Khatamun-Nabiyyin (Mtume wa mwisho).”Suratul Ahzaab 33:40.
Imani ya Akhera hujenga uwajibikaji wa matendo: “Na hakika Saa itakuja, haina shaka; na Mwenyezi Mungu atawafufua waliomo makaburini.”Suratul Hajj 22:7.
Aqiydah sahihi inajumuisha kumuamini Qadar, kheri na shari yake: “Hakika Sisi tumeumba kila kitu kwa kipimo.”Suratul Qamar 54:49. Itikadi ya kweli huonekana katika matendo.
“Hakika wale walioamini na wakatenda mema, watapata Pepo.”Suratul Kahf 18:107. Imani isiyozaa tabia njema si imani kamilifu.
Hata hivyo, Qur’ani Inakataza Kupindukia Katika Itikadi, Aqiydah sahihi ni ya wastani Qur’ani Tukufu inaeleza kuwa; “Wala msipite mipaka katika dini yenu.”Suratun-Nisaa 4:171.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, Aqiydah sahihi ya Kiislamu inajengwa juu ya Tauhidi ya kweli, kumuamini Mwenyezi Mungu, Malaika, Vitabu, Mitume, Siku ya Mwisho na Qadar, kufuata Qur’ani na Sunnah kwa uelewa sahihi, na kuishi kwa maadili mema.
Hii ndiyo Aqiydah inayomlinda Muislamu duniani na kumwongoza kuelekea radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo Akhera.
0 Comments