NGUZO TANO ZA UISLAMU NI MFUMO WA MAISHA YA KAWAIDA KWA WAUMINI
Na Amina A. Juma
As-salāmu ‘alaykum wa raḥmatullāhi wa barakātuh! Uislamu si ibada za msikitini pekee, bali ni mfumo kamili wa maisha unaomwongoza Muislamu katika imani, maadili, ibada, mahusiano na ustawi wa jamii. Nguzo Tano za Uislamu ndizo msingi wa mfumo huu; zinamjenga mja kiroho, kimwili na kijamii, na kumfanya aishi maisha yenye nidhamu, uadilifu na amani. Qur’ani Tukufu imeweka dalili na misingi ya kila nguzo ili iwe mwongozo wa maisha ya kila siku ya Waumini.
Shahada ni Msingi wa Imani na Mwelekeo wa Maisha, Shahada humweka Muislamu katika mwelekeo sahihi wa kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja na kufuata Mtume Wake. “Mwenyezi Mungu ameshuhudia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Yeye…”Suratu Aal ‘Imraan 3:18.
“Muhammad si baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”Suratul Ahzaab 33:40. Shahada humjenga Muislamu awe na kusudio sahihi katika kila tendo la maisha.
Swala ni Nidhamu na Kumbukumbu ya Mola Katika Maisha ya Kila Siku. Swala ni nguzo ya pili na nguzo ya nidhamu ya kila siku. “Hakika Swala humzuilia mtu na machafu na maovu.”Suratul ‘Ankabut 29:45.
“Hakika Swala imefaradhishwa juu ya Waumini kwa nyakati maalumu.”Suratun-Nisaa 4:103. Swala humjenga Muislamu kuwa na ratiba, maadili mema na uhusiano wa kudumu na Mola wake.
Zaka ni Msingi wa Haki ya Kijamii na Ustawi, aidha zaka huunganisha ibada na haki za kijamii. “Na simamisheni Swala na toeni Zaka.”Suratul Baqarah 2:110. “Chukua katika mali zao Zaka; uwatakase na kuwatakasia kwa hiyo.”Suratut-Tawbah 9:103. Zaka hupunguza umaskini, huimarisha mshikamano na kusafisha mali na nafsi.
Saumu ya Ramadhani ni Mafunzo ya Nidhamu na Uchamungu, saumu humjenga Muislamu ajidhibiti na kuwa na huruma. “Enyi mlioamini! Mmefaradhiwa Saumu kama walivyofaradhiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate uchamungu.”Suratul Baqarah 2:183. Saumu huathiri maisha ya kawaida kwa kujenga subira, nidhamu na uangalifu wa matendo.
Hija ni Umoja, Usawa na Kumbukumbu ya Akhera, Hija huonyesha usawa wa binadamu na umoja wa Umma. “Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibika kwa watu kuhiji Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kwenda huko.”Suratu Aal ‘Imraan 3:97. Hija humkumbusha Muislamu unyenyekevu, nidhamu na uwajibikaji wa kijamii na kiroho.
Nguzo Tano kama Mfumo wa Maisha ya Kawaida kwa pamoja, Nguzo Tano huimarisha imani (Shahada), huweka nidhamu ya kila siku (Swala), hujenga haki ya kijamii (Zaka), hulea maadili na subira (Saumu), na huimarisha umoja na usawa (Hija).
“Na hivyo tumekufanyeni muwe umma wa wastani.”Suratul Baqarah 2:143. Huu ndio mfumo wa maisha ya kawaida ya Muislamu: wa kati, wa haki na wa rehema.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, Nguzo Tano za Uislamu ni mfumo kamili wa maisha ya Waumini, unaogusa kila nyanja ya maisha—imani, ibada, maadili na jamii. Kuzitekeleza kwa uelewa na ikhlasi kunamjenga Muislamu kuwa raia mwema, mja mnyenyekevu na mjenzi wa amani katika jamii.
0 Comments