UTULIVU WA NAFSI NI MATUNDA YA DARAJA LA IMANI NA KUMTAMBUA MOLA
Na Amina A. Juma
Wa ‘alaykumus-salām wa raḥmatullāhi wa barakātuh!, Alhamdulillāh, Nudu zangu Katika maisha ya mwanadamu, changamoto, misukosuko na mitihani ni sehemu ya safari ya duniani. Watu wengi hutafuta utulivu wa nafsi kupitia mali, cheo au starehe, lakini mara nyingi hawaupati. Qur’ani Tukufu inafundisha kuwa utulivu wa kweli wa nafsi haupatikani isipokuwa kwa imani ya kweli na kumtambua Mwenyezi Mungu (Mola). Kadiri imani ya mja inavyoongezeka, ndivyo moyo wake unavyopata amani na faraja.
Qur’ani inaweka msingi wa wazi kuhusu chanzo cha utulivu wa moyo: “Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndiko kunakotuliza nyoyo.” Suratur-Ra‘d 13:28. Aya hii inaonyesha kuwa dhikri, dua na kumuamini Mwenyezi Mungu ndizo nguzo kuu za utulivu wa nafsi.
Mtu mwenye imani thabiti huwa na matumaini na subira katika kila hali: “Bila shaka wale walioamini na wakawa wakimcha Mwenyezi Mungu, hawatakuwa na hofu wala hawatahuzunika.” Suratu Yunus 10:62. Hii inaonesha kuwa daraja la imani humsaidia mja kuishi kwa amani ya moyo hata anapokabiliwa na mitihani.
Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa waumini: “Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza kwenye nuru.” — Suratul Baqarah 2:257, Kumtambua Mwenyezi Mungu kama Mlinzi humjengea mja utulivu wa nafsi na kuondoa hofu ya kupotea au kudhulumiwa.
Subira na Swala ni Njia ya Kutuliza Nafsi, Qur’ani inawapa waumini muongozo wa vitendo: “Na tafuteni msaada kwa subira na swala; na hakika swala ni nzito isipokuwa kwa wanyenyekevu.” Suratul Baqarah 2:45. Subira na swala humuunganisha mja na Mola wake, na hivyo kumletea faraja na utulivu wa moyo.
Nafsi Tuli ni Kiwango cha Imani Iliyokamilika katika uwislamu, Qur’ani inaitaja nafsi iliyofikia utulivu kama daraja la juu: “Ewe nafsi iliyotulia! Rudi kwa Mola wako hali ya kuwa umeridhika na umemeridhiwa.” Suratul Fajr 89:27–28. Aya hii inaonesha kuwa utulivu wa nafsi ni matunda ya imani iliyokomaa na uhusiano mzuri kati ya mja na Mola wake.
Mwislamu aliyekamilika siku zote Kumtegemea Mwenyezi Mungu kwani Huondoa Msongo wa Mawazo. Tawakkul (kumtegemea Mwenyezi Mungu) huleta amani ya ndani: “Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu basi Yeye humtosha.” Suratut-Talaaq 65:3. Mtu anayemtegemea Mwenyezi Mungu huishi kwa utulivu bila hofu ya kupita kiasi juu ya riziki na mustakabali wake.
Mwenyezi Mungu anaeleza wazi kuwa Qur’ani ni Tiba ya Moyo na Nafsi: “Na tunateremsha katika Qur’ani yaliyo tiba na rehema kwa Waumini.” Suratul Israa 17:82. Kusoma, kutafakari na kuifuata Qur’ani huponya maumivu ya nafsi na kuleta utulivu wa kweli.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, utulivu wa nafsi si bahati wala matokeo ya mali, bali ni tunda la daraja la imani na kumtambua Mwenyezi Mungu kwa haki. Moyo unaotulia ni moyo unaomkumbuka Mwenyezi Mungu mara kwa mara, unaoamini Qadar ya Mola, unaotekeleza ibada kwa ikhlasi,na unaotegemea rehema za Mwenyezi Mungu.
Hivyo, Waislamu wanapaswa kuimarisha imani zao na uhusiano wao na Mwenyezi Mungu ili kupata utulivu wa nafsi hapa duniani na mafanikio ya Akhera.
0 Comments