ATHARI ZA KUWA NA ITIKADI ZA IMANI KALI KWA MUJIBU WA QUR’ANI TUKUFU
Na Haseeb S Izaan
Itikadi za imani kali ni misimamo ya kupindukia katika masuala ya dini, ambapo mtu huvuka mipaka ya mafundisho sahihi ya Mwenyezi Mungu kwa kuongeza, kupunguza au kupotosha ukweli wa dini. Uislamu ni dini ya mizani, hekima na wastani. Mwenyezi Mungu ameweka misingi ya dini kwa uwiano unaolinda haki za binadamu, amani ya jamii na usafi wa itikadi. Qur’ani Tukufu inatoa onyo na mwongozo wa wazi dhidi ya misimamo hiyo.
Athari kubwa ya imani kali ni kuvuruga msingi wa Tauhidi. Qur’ani inaonya dhidi ya kupindukia katika dini: “Enyi Watu wa Kitabu! Msipite mipaka katika dini yenu…”Suratun Nisaa 4:171. Kupindukia humpeleka mtu ama kuongeza mambo yasiyo katika dini au kupotosha maana ya kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa usahihi.
Watu wenye imani kali mara nyingi huchukua sehemu ya maandiko na kuyaacha mengine, hali inayosababisha upotovu: “Je, mnaamini sehemu ya Kitabu na mnakataa sehemu nyingine?”Suratul Baqarah 2:85. Hii ni dalili kuwa imani kali huondoa uadilifu wa uelewa wa Qur’ani na Sunnah kwa ujumla wake.
Qur’ani inahimiza umoja, lakini imani kali huleta mifarakano: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote kwa pamoja, wala msifarakane.”Suratu Aal Imraan 3:103. Migawanyiko mingi ya kidini hutokana na misimamo mikali inayokosa hekima na subira.
Wenye imani kali mara nyingi hujihalalishia dhuluma kwa madai ya kutetea dini. Qur’ani inakataza hilo wazi: “Na wala chuki ya watu isiwapelekee kutotenda uadilifu. Tendeni uadilifu; huo ndio karibu zaidi na uchamungu.”Suratul Maa’idah 5:8. Uislamu haukubali dhuluma kwa kisingizio chochote.
Msingi wa Uislamu ni rehema, lakini imani kali huondoa huruma mioyoni: “Na hatukukutuma (Muhammad) ila uwe rehema kwa walimwengu wote.”Suratul Anbiyaa 21:107. Kukosa rehema ni dalili ya uelewa potofu wa dini.
Qur’ani inakataza kusema au kuhukumu bila elimu: “Wala usiyafuate mambo usiyo na elimu nayo.”Suratul Israa 17:36. Imani kali huwafanya watu kutoa hukumu nzito bila maarifa ya kina ya dini.
Matendo ya kupindukia huwafanya watu kuichukia au kuikosea tafsiri dini: “Na hivyo tumekufanyeni muwe umma wa wastani.”Suratul Baqarah 2:143. Uislamu wa kweli ni wa wastani, unaovutia na kuleta amani.
Mwenyezi Mungu anatoa mwongozo wa kutumia hekima katika dini: “Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri.”Suratun Nahl 16:125. Hekima na mawaidha mema ni silaha za Uislamu, si ukali na kulazimisha.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, itikadi za imani kali zina athari mbaya kwa mtu binafsi, jamii na dini kwa ujumla. Husababisha upotovu wa itikadi, migawanyiko ya kijamii, dhuluma na chuki, na kuharibika kwa taswira ya Uislamu.
Uislamu unatufundisha njia ya wastani, uadilifu, hekima na rehema. Waislamu wanapaswa kujiepusha na misimamo mikali na kushikamana na Qur’ani na Sunnah kwa uelewa mpana na sahihi, ili dini ibaki kuwa chanzo cha amani na uongofu kwa wanadamu wote.
1 Comments