Katika maisha ya kila siku, maneno yana nguvu kubwa yanaweza kujenga au kubomoa, kuleta amani au kusababisha migogoro. Dini ya Kiislamu imetoa maelekezo ya kina kuhusu matumizi ya ulimi na umuhimu wa kunyamaza pale inapohitajika. Qur’ani Tukufu inawahimiza Waislamu kutumia busara katika maneno yao na kunyamaza pale ambapo kunena kungeleta madhara.
Mtume Muhammad (SAW) alihimiza umma wake kuzingatia maneo yao na kuchagua wakati sahihi wa kuzungumza. Msingi wa maadili ya Kiislamu ni kunena yaliyo mema na yenye faida. Pale ambapo maneno hayana kheri, kunyamaza ni ibada: “Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno yaliyo sawa.”Suratul Ahzab 33:70
Aya hii inafundisha kuwa si kila jambo linahitaji kusemwa. Maneno yasiyo ya haki, ya uchochezi au ya uongo hayana nafasi katika maisha ya Muislamu. Kunyamaza hulinda heshima ya mtu na jamii kwa ujumla.
Fitina, uzushi na udaku ni miongoni mwa vitendo viovu vinavyoharibu jamii. Qur’ani inatoa onyo kali dhidi ya kusambaza habari bila uhakika: “Enyi mlioamini! Mnapoletwa na mpotovu habari, ichunguzeni…”Suratul Hujurat 49:6
Aya hii inawahimiza Waislamu kujizuia kunena au kusambaza maneno yanayoweza kuleta madhara. Katika mazingira ya sasa, hususan kupitia mitandao ya kijamii, kunyamaza kabla ya kuthibitisha taarifa ni kinga dhidi ya dhambi na machafuko.
Moja ya sababu kubwa za migogoro katika jamii ni matumizi ya lugha chafu na ya kudhalilisha wengine. Qur’ani inasema: “Enyi mlioamini! Watu wasiwadharau watu wengine… wala msitukanane kwa majina mabaya.”Suratul Hujurat 49:11
Aya hii inawahimiza Waislamu wa Tanzania kuachana na matusi, kejeli na lugha za chuki iwe ni katika familia, mitaani, au kwenye majukwaa ya umma. Kunyamaza katika hali ya hasira ni njia ya kulinda amani.
Maneno mengi yasiyo na faida humpeleka mtu katika dhambi bila yeye kutambua. Qur’ani inawakumbusha waumini kuwa kila neno linahesabiwa:
“Hatatamka neno lolote ila kuna mwangalizi aliye tayari (kuandika).”Suratul Qaaf 50:18
Aya hii inamfanya Muislamu atafakari kabla ya kuzungumza. Kunyamaza pale ambapo maneno hayana manufaa ni njia ya kujilinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Mara nyingi, maneno mabaya hutoka katika hasira. Uislamu unahimiza subira na udhibiti wa nafsi: “…na wanaojizuia hasira na kuwasamehe watu.”Suratu Aal Imraan 3:134
Kunyamaza wakati wa hasira ni dalili ya imani na ukomavu wa kiroho. Jamii inayojifunza kunyamaza badala ya kulipiza kwa maneno, hujenga amani na mshikamano.
Vitendo viovu kama uchochezi, ugomvi, udaku, uzushi, na migawanyiko ya kikabila au kidini huanzia kwenye maneno. Qur’ani inasema: “Na waambie waja wangu waseme yaliyo bora.”Suratul Israa 17:53
Aya hii inawahimiza Waislamu kuchagua maneno bora au kunyamaza kabisa ili kuepuka Shetani kuingilia na kuleta uovu. Kwa kufanya hivyo, jamii ya Watanzania inaweza kudumisha amani, heshima na umoja.
Uislamu haumhimizi Muislamu azungumze kila mara, bali azungumze kwa hekima: “Na usifuate usiyoyajua; hakika masikio, macho na moyo, vyote vitaulizwa.”Suratul Israa 17:36
Hii inaonyesha kuwa kunyamaza pale ambapo mtu hana elimu ya jambo ni ibada na ni njia ya kujiepusha na dhambi.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, kunyamaza ni maadili muhimu katika Uislamu na ni silaha madhubuti ya kupambana na vitendo viovu katika jamii. Kunyamaza hulinda heshima ya mtu na jamii, huzuia fitina, uongo, hujenga subira na amani na humweka Muislamu karibu na radhi za Mwenyezi Mungu.
Kwa Waislamu wa Tanzania, ni wakati wa kurejea mafunzo ya Qur’ani kwa vitendo kusema mema au kunyamazaili kujenga jamii yenye maadili, umoja na hofu ya Mwenyezi Mungu.
0 Comments