Uislamu ni dini inayojenga maisha ya jamii juu ya misingi ya nidhamu, uadilifu na utulivu. Ili jamii iweze kuishi kwa amani, ni lazima kuwepo na mamlaka yanayosimamia sheria, haki na usalama. Qur’ani Tukufu, kama chanzo kikuu cha mafunzo ya Kiislamu, inawahimiza Waislamu kuheshimu mamlaka halali za nchi, kuzitii sheria kwa wema, na kuepuka machafuko.
Makala hii imelenga kueleza kwa kina jinsi Uislamu unavyohimiza kuheshimu mamlaka za nchi kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu. Qur’ani inaweka wazi wajibu wa waumini kuwatii viongozi waliowekwa kusimamia jamii, mradi wasiamrishe uovu: “Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume, na wenye mamlaka miongoni mwenu…”— Suratun Nisaa 4:59
Aya hii inaonyesha kuwa utii kwa viongozi wa nchi ni sehemu ya utii wa kijamii unaolenga kudumisha utulivu na mshikamano. Uislamu hautaki jamii isiyo na uongozi, kwani hali hiyo husababisha vurugu na ukosefu wa haki.
Kuvunja mamlaka halali mara nyingi husababisha fitina na uharibifu. Qur’ani inawakataza waumini kufanya uharibifu katika ardhi: “Wala msifanye uharibifu katika ardhi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa.”— Suratul A‘raf 7:56
Hii inaonyesha kuwa Uislamu hauungi mkono vitendo vinavyovuruga amani ya nchi, kama uasi wa vurugu au chuki dhidi ya mamlaka bila msingi wa haki.
Qur’ani inaeleza kuwa mamlaka na uongozi ni sehemu ya mpangilio wa Mwenyezi Mungu kwa ustawi wa wanadamu: “Sema: Ee Mwenyezi Mungu! Wewe ndiye Mmiliki wa mamlaka; humpa mamlaka umtakaye na humwondolea umtakaye…”— Suratu Aal Imraan 3:26. Aya hii inamkumbusha Muislamu kuwa kuheshimu mamlaka ni kutambua mpango wa Mwenyezi Mungu katika uendeshaji wa dunia.
Sheria za nchi zinalenga kulinda haki na usalama wa raia. Qur’ani inaamuru watu washikamane na haki na nidhamu: “Hakika Mwenyezi Mungu anaamuru uadilifu na ihsani…”— Suratun Nahl 16:90. Utii kwa mamlaka na sheria halali husaidia kutekeleza uadilifu huu unaoelekezwa na Qur’ani.
Kumekuwa na tabia ya baadi ya waislamu kujichukulia sheria mkononi, badala ya kuchukua sheria mikononi, Qur’ani inawaelekeza waumini kurejea mamlaka na sheria pale panapotokea tofauti: “Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume…”— Suratun Nisaa 4:59
Hii inaonyesha kuwa Uislamu unakataa vurugu na kulipiza kisasi binafsi, bali unahimiza utatuzi wa migogoro kwa njia halali.
Qur’ani inasisitiza umuhimu wa usalama kama neema ya Mwenyezi Mungu: “Ambaye amewalisha kutokana na njaa na akawalinda na hofu.”— Suratul Quraysh 106:4
Usalama huu hauwezi kupatikana bila kuheshimu mamlaka zinazolinda amani ya nchi. Hivyo, Uislamu unawahimiza waumini kuunga mkono jitihada za mamlaka katika kudumisha usalama. Qur’ani inaonya dhidi ya mgawanyiko na kuvunja umoja wa jamii: “Wala msigombane msije mkavunjika nguvu zenu…”— Suratul Anfal 8:46
Uasi na dharau dhidi ya mamlaka mara nyingi husababisha migawanyiko na kudhoofisha taifa, jambo ambalo Uislamu hauliruhusu.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, ni wazi kuwa Uislamu unahimiza kuheshimu mamlaka za nchi kama sehemu ya kulinda amani, usalama na uadilifu katika jamii. Kwa hiyo, Muislamu wa kweli ni yule anayeheshimu sheria na mamlaka za nchi anayoishi, akitafuta haki kwa njia za amani na halali, bila kuvuruga utulivu wa jamii.
0 Comments