Katika karne ya sasa, vitendo vya ugaidi vimekuwa vikipewa sura ya kidini na mara nyingi kuhusishwa na Uislamu. Hii ni taswira potofu na isiyo na msingi. Uislamu, kama ilivyo dini nyingine za haki na maadili, unasisitiza amani, uadilifu, na utunzaji wa uhai wa binadamu. Qur’ani Tukufu chanzo kikuu cha sheria na mafunzo ya Kiislamu inaonyesha kwa uwazi kuwa uhalifu, mauaji ya kiholela, na uonevu havina nafasi katika mafundisho ya dini.
Aya mojawapo mashuhuri zaidi inayokataza mauaji yasiyo na sababu ni ile inayolinganishwa na thamani ya uhai wa mwanadamu: “…Atakayeuua mtu asiyekuwa na hatia… ni kama ameua watu wote.”Suratul Maida 5:32.
Aya hii inaweka msimamo bayana kuwa uhai wa mwanadamu hauruhusiwi kuondolewa kiholela. Ugaidi ni vitendo vinavyolenga kuua, kuumiza au kuwatisha raia hivyo vinakwenda kinyume kabisa na agizo hili.
Wapo wanaotumia vibaya mada ya Jihadi kwa kutenda ugaidi, ilhali Qur’ani inaweka mipaka mikali: “Piganeni na wale wanaowapiga, lakini msivuke mipaka, kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wanaovuka mipaka.” Suratul Baqarah 2:190.
Hii inaonyesha kuwa hata katika hali ya vita halali, Waislamu hawaruhusiwi kuanzisha mashambulizi ya kigaidi, kuwadhuru wasiopigana, au kutenda uovu kwa kisingizio cha dini. Mwenyezi Mungu anawaamrisha Waislamu kuishi kwa amani na wale wasiowapiga vita: “Mwenyezi Mungu hakujizuieni na wale wasiokupigeni vita… kuwa watendeeni wema na uadilifu.” Suratul Mumtahanah 60:8.
Aya hii inathibitisha kuwa mahusiano ya mwanzo ya Muislamu na wengine ni amani, si uadui, vitisho, wala fujo.
Uislamu unakana kwa nguvu fikra za kutumia ghasia katika kueneza dini: “Waitie watu katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri…” Suratun Nahl 16:125. Hakuna mahali Qur’an inaruhusu kulazimisha watu kwa mabavu, kuwatisha, au kuwaumiza. Hivyo, ugaidi wa kuwalazimisha watu waogope au wakubali jambo ni mbali sana na Uislamu.
Qur’ani pia inasema: “Fitina (uchochezi na uharibifu) ni mbaya zaidi kuliko kuua.” Suratul Baqarah 2:191. Ugaidi ni fitina kwa kiwango kikubwa uneneaji wa hofu, uharibifu wa mali, na kusababisha vurugu. Uislamu unakemea kwa nguvu aina yoyote ya uharibifu wa jamii.
Neno “Islam” lenyewe linatokana na mzizi wa Kiarabu “salama” lenye maana ya amani. Mtume Muhammad (rehema na amani zimfikie) amesisitiza: “Muislamu ni yule ambaye watu wako salama kutokana na ulimi na mikono yake.” Hili linaonyesha kuwa Muislamu wa kweli hawezi kuwa chanzo cha hofu wala ugaidi.
Mafundisho ya Qur’ani yanatoa msimamo thabiti na usio na utata: ugaidi hauna uhusiano wowote na Uislamu au dini yoyote ya haki. Vitendo vya kigaidi ni matokeo ya misimamo mikali, siasa, chuki, ujinga, au matumizi mabaya ya dini kwa faida binafsi.
Dunia inapaswa kutofautisha kati ya mafundisho safi ya dini na vitendo vya wachache wanaopotosha ujumbe huo. Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, uhai wa mtu ni wa thamani kubwa mno, amani ni msingi mkuu wa maisha ya kijamii, na uadilifu ni nguzo ya udugu wa binadamu.
0 Comments