Katika Uislamu, mema tunayowatakia wengine si sadaka ya maneno tu ni ibada ambayo inaleta kheri kwa anayetamkiwa na zaidi kwa anayetenda. Huu ni msingi uliojengwa moja kwa moja na Qur’an na mafundisho ya Mtume, mtu akifanya mema kwa wengine, Allah humletea mema zaidi yeye mwenyewe, kwa njia anazozijua Yeye.
Allah anatukumbusha kuwa Waislamu wanapaswa kushirikiana katika mema na kuzuia mabaya. Aya mashuhuri inasema; “Na saidianeni katika wema na uchamungu.” (Qur’an 5:2)
Kupigania mema kwa wengine, kutamani waongoke, wafaulu, wapate riziki njema, au walindwe na Allah—haya ni sehemu ya kusaidiana katika wema. Na kila tendo la wema, hata kama ni kwa maneno, halipotei mbele ya Mola.
Du’a kwa wengine ni moja ya matendo yanayopendwa sana katika Uislamu. Qur’an inatufundisha kuwa dua haipotei, bali huamsha rehema: “Mola wenu anasema: Niombeni, nitakujibuni.” (Qur’an 40:60)
Wakati unamwombea mwenzako afanikiwe, Allah hukujibu kwanza kwa kukuandikia thawabu na kheri. Kwa sababu du’a ni ukarimu wa kiroho na Allah huwapa wakarimu zaidi kuliko walivyotoa.
Qur’an inathibitisha kuwa kila tendo la kheri humrudia mtendaaji wake kwa njia bora na kubwa zaidi: “Atendaye wema, hujifanyia nafsi yake; na atendaye uovu, hujifanyia nafsi yake.” (Qur’an 45:15)
Ukisemea mema, unajipatia mema. Ukitamani watu wafaulu, nawe unajikaribia kufaulu. Ukibariki riziki ya mwenzako, yako pia inafunguliwa. Huu ni mfumo wa Allah wa uadilifu na rehema.
Qur’an inauinua sana moyo ulio safi, uliojaa nia njema kwa watu: “Siku ambayo mali wala watoto havitofaa kitu, isipokuwa mwenye kumletea Allah moyo uliosalimika.” (Qur’an 26:88–89)
Moyo unaotamani mema kwa wengine haujengeki kwa kinyongo, husda, au chuki. Ni moyo unaosalimika—na Allah ameuahidi heshima mbele Yake.
Mmoja wa tabia muhimu za waumini ni uwema na ukarimu. Qur’an inawasifia wale wanaowatakia wengine mema hata wanapokuwa na machache; “Na wanawapendelea wengine kuliko nafsi zao, ijapokuwa wao wenyewe wana uhitaji.” (Qur’an 59:9)
Hii ni ahadi moja kwa moja: ukimtakia mwenzako mema, hata kama wewe bado hupati hayo mema, Allah atakujia kwa wakati wake na mara nyingi huja kwa namna iliyo bora kuliko ulivyotarajia.
Kauli “Ukimtakia mwenzako mema, Allah anakupa wewe kwanza” si methali tu; ni ukweli unaotiririka ndani ya Qur’an na misingi ya Uislamu.
Mja mwenye tabia ya kuwatakia wengine kheri moyo wake unasafishwa, du’a zake zinajibiwa, riziki yake inazidishwa na nafasi yake mbele ya Allah inainuliwa. Kwa hivyo, kila unapomwambia mwenzako “Allah akupe kheri”, tambua kuwa unajifungulia milango ya kheri zako pia.
1 Comments