Uislamu ni dini ya amani, uadilifu na uwajibikaji. Muislamu anawajibika kuishi kwa kuleta manufaa katika jamii na kuilinda nchi yake dhidi ya mambo yote yanayoweza kusababisha migogoro, uharibifu au kuvuruga utulivu. Upendo kwa nchi si suala la uchaguzi bali ni jukumu la kidini na kiubinadamu, kwani nchi ndiyo mahali tunapoishi, tunapopata riziki, tunapoabudu na ku tafuta maendeleo.
Qur’an inasisitiza mara nyingi umuhimu wa amani na kutenda mema katika jamii. Allaah anasema; “Na Allah anawaamuru uadilifu, ihsani na kuwapa jamaa haki zao, na anawakataza machafu, maovu na uasi.” (Qur’an 16:90). Aya hii inaweka msingi wa ustawi wa jamii: uadilifu, fadhila na kuepuka uovu. Msingi huu hauwezi kutimia bila amani na utulivu wa nchi.
Pia Mwenyezi Mungu anasema; “Wala msilete uharibifu katika ardhi baada ya kuwa imekwishatengenezwa.” (Qur’an 7:56). Aya hii inakataza vitendo vyote vinavyoharibu amani, utulivu na maendeleo ya nchi. Hivyo, Muislamu anatakiwa kuwa mtu wa kulinda, si kuvuruga.
Mapenzi kwa nchi (hubbul-watan) ni tabia iliyokubaliwa katika Uislamu. Mtume Muhammad (S.A.W) alionyesha mapenzi makubwa kwa Makka alipoihama kwenda Madina. Alisema; “Ewe Makka! Hakuna mahali penye kupendwa zaidi kwangu kuliko wewe.” Hii inaonyesha kuwa kupenda nchi ni jambo la asili kwa muislamu na linaendana na maadili ya Kiislamu.
Qur’an inatufundisha kushirikiana katika mambo ya kheri na siyo uhalifu au uharibifu. Mwenyezi Mungu asema; “Na shirikianeni katika wema na uchamungu, wala msishirikiane katika dhambi na uadui.” (Qur’an 5:2)
Kulinda amani ni miongoni mwa “wema na uchamungu”. Muislamu anatakiwa kuwa chanzo cha utulivu kwenye familia, shule, mtaa na taifa. Hatakiwi kushiriki au kuchochea mambo yanayosababisha mgawanyiko, vurugu au chuki. Mtume (S.A.W) pia alisema; “Muislamu ni yule ambaye Waislamu wengine wako salama kwa ulimi wake na mkono wake.”Hadith hii inaipa thamani kubwa amani kwani Muislamu anatakiwa awe mtu wa kuleta usalama kwa wengine, si hatari.
Amani ni miongoni mwa neema kubwa zilizotajwa na Qur’an. Bila amani hakuna elimu, uchumi, afya wala ibada kwa utulivu. Mwenyezi Mungu anatukumbusha; “Basi na wamwabudu Mola wa Nyumba hii (Al-Kaaba), ambaye amewapa kula njaa yao na amewapa amani baada ya hofu.”(Qur’an 106:3–4).Hii inaonyesha kuwa amani ni zawadi na wajibu wa kuitunza.
Vijana wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa. Kwa Muislamu kijana, kulinda amani kunahusisha Kufanya mazungumzo ya upole na kuheshimiana, Kuepuka ushawishi wa vurugu au makundi ya uhalifu, Kutumia mitandao ya kijamii kwa busara bila kuchochea chuki, Kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii, Kutii sheria za nchi na kuheshimu viongozi. Uislamu unataka vijana wawe nguzo za maendeleo, sio chanzo cha migogoro.
Kuipenda nchi na kulinda amani ni jukumu muhimu kwa kila Muislamu. Qur’an na Sunna zimeweka wazi kwamba uharibifu, fitna, vurugu na uadui havina nafasi katika maisha ya Kiislamu. Muislamu anapaswa kuwa kielelezo cha uadilifu, upendo, kujenga nchi, na kulinda neema za Mwenyezi Mungu hasa amani.
Amani inaanza na mimi, wewe na kila mmoja wetu. Kulinda amani ni njia ya kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu na kutekeleza mafundisho ya Uislamu.
0 Comments