WAISLAMU TUSIKUBALI KUTUMIKA NA MATAIFA YA MAGHARIBI KUVURUGA AMANI
Na Haseeb S Izaan
Katika karne ya leo, dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiusalama. Nchi zenye nguvu iwe za Magharibi au Mashariki mara nyingi zinatafuta ushawishi katika mataifa mengine kwa malengo ya kisiasa, kimkakati au kiuchumi. Katika mazingira haya, jamii zisizokuwa na umoja au msimamo thabiti huwa rahisi kutumiwa kama nyenzo za kuendeleza migogoro, mafarakano au machafuko.
Kwa Waislamu, hili ni jambo linalohitaji umakini mkubwa, kwa sababu Uislamu unasisitiza sana uadilifu, amani, umoja na kutokubali udanganyifu. Qur’an na Sunna zinatupatia misingi imara ya kutambua, kukataa na kuepuka mipango yoyote ya kutumiwa vibaya.
Uislamu wenyewe ni dini ya amani, mizani na uadilifu, na unapoweka msingi wa maamuzi katika misingi ya Qur’an na Sunna, unazuia mtu au jamii kuingia katika mivutano isiyo na manufaa, hasa ile inayoendeshwa na maslahi ya mataifa ya nje.
Katika zama za taarifa nyingi, taarifa potofu ni rahisi kusambaa na kuathiri fikra za watu. Qur’an inatuonya kuhusu kufuata mambo bila ujuzi: “Wala msifuate mambo ambayo hamna ujuzi nayo…”(Qur’an 17:36).
Aya hii si tu nasaha ya kiimani, bali pia inatufundisha maadili ya kiakili, kufanya uchunguzi, kutotawaliwa na hisia, na kutofanya maamuzi kwa misukumo ya nje. Mataifa yenye maslahi ya kisiasa hutumia propaganda, taarifa zilizotengenezwa na mbinu za kisaikolojia ili kuathiri mitazamo ya jamii fulani dhidi ya jamii nyingine.
Kwa hiyo, Waislamu wanapaswa kuwa makini na wachambuzi wazuri wa taarifa, si wafuasi wa masimulizi yanayodhamiria kuleta mfarakano ndani ya umma. Mwenyezi Mungu anatuamrisha; “Na shikamaneni wote kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu, wala msifarakiane.” (Qur’an 3:103).
Mgawanyiko wa Waislamu ni moja ya maeneo ambayo mataifa makubwa mara nyingi huyaendea. Wanasaidia makundi yanayokinzana, wanapandikiza chuki za kimadhehebu, wanakuza migawanyiko ya kikabila au kisiasa, hadi jamii inageuka kuwa dhaifu na isiyoweza kujiamulia mustakabali wake.
Umoja wa Waislamu hauimaanishi kufanana katika kila jambo, bali kuheshimiana, kusameheana, kuepuka matamshi ya chuki na kutanguliza maslahi ya pamoja. Wakati umma unakuwa na mshikamano, nguvu za nje haziwezi kuutumia kama chombo.
Ingawa dunia ina migogoro mingi, Uislamu haujawahi kuruhusu kushiriki katika ghasia zisizo na msingi wa uadilifu. Allaah anasema; “Na msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha kutengenezwa.” (Qur’an 7:56)
Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’an, Waislamu tunahaswa kujiepushe na vitendo vinavyoharibu nyumba, familia, uchumi na maisha ya wanawake, vijana na watoto. Kulinda amani ni ibada. Kuvunja amani bila sababu za haki ni kukiuka amri ya Mwenyezi Mungu.
Waislamu, kwa kuwa na mafundisho ya Qur’an, wanapaswa kuwa watu wanaotathmini hali za kisiasa kwa uadilifu. Uislamu haukatazi siasa; unakataza udhalimu, upotoshaji na kutumiwa kuharibu wengine. Wakati wowote ambapo taifa au kundi linahimizwa kuchukua hatua za kufanya vurugu, Waislamu wanapaswa kujiuliza mambo yafuatayo; ”Ni nani ananufaika?, Ni nani atakaeumia?, Je, hatua hii inaendana na Qur’an na Sunna?, Je, inalinda amani, au inaleta maangamizi?”.
Uislamu ni dini ya upatanisho. Hata katikati ya tofauti, Qur’an inawahimiza Waislamu kuchagua amani inapowezekana; “Na ikiwa wanaelekea kwenye amani, nawe pia elekea kwenye amani…” (Qur’an 8:61).
Tofauti kati ya mataifa au makundi ndani ya jamii si lazima ziishie katika migogoro. Mazungumzo, uwazi, uadilifu na kusameheana ni njia ambazo Qur’an inazipa kipaumbele.
Mara nyingi, mataifa makubwa hujaribu kuleta chuki kwa wananchi kwa kutumia wanaharakari na baaadhi ya vyama vya kisiasa kwa sababu yanapata faida kiuchumi hasa wakigundua nchi lengwa inarasilimali za kutosha. Kwa hiyo, mshikamano na busara ya Waislamu ni ngao dhidi ya kutumiwa katika mipango kama hiyo.
Uislamu unahimiza elimu, uchambuzi na ufahamu. Mtume Muhammad (s.a.w.) alisisitiza kusoma, kuchunguza, kujadili na kufikiri kwa kina. Haya ni mambo yanayofanya jamii kuwa thabiti na isiyotawaliwa na propaganda za nje.
Katika dunia ya leo, ambapo nguvu za kigeni zinatafuta maslahi kwa njia zote, Waislamu wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda Amani, Uadilifu, Umoja, Uchambuzi wa kina, Maadili ya Kiislamu. Kwa kufanya hivyo, hatutakuwa rahisi kutumiwa kama nyenzo za kuleta machafuko. Badala yake, tutakuwa jamii inayojenga amani na uadilifu kama Qur’an inavyotuongoza.
0 Comments