KWA hakika kila mwadilifu anapoangalia historia ya ulimwengu huu tangu kuumbwa kwa Mwanadamu, atatambua kuwa haifai kwa njia zozote kunasibisha uhalifu ama ugaidi kwa kutumia kisingizio cha dini, Madhehebu, Taifa au Nchi kwa sababu dini hazikuteremshwa isipokuwa kwa kueneza usalama, amani na upendo baina ya wanadamu wote.
Tukiangalia kwa makini vile vyanzo vya ualifu au ugaidi tutagundua kwamba una misingi mbali mbali lakini kuna misingi mikuu miwili ambayo ni kuwa na misimamo na itikadi kali katika dini, madhebu, au taifa fulani.
Hali kimaisha kwa katika jamii, uelewa kifikra, kimafundisho na kijamii kwa ujumla ambapo vijana ndiyo walengwa wakuu wa vikundi vya kigaidi wanatumia baaadhi ya mafundisho kuwalaghai na kuwachonganisha na Serikali zao ikiwa ni maandalizi ya kutaka vijana kujiunga ili kuongeza nguvu katika makundi hayo.
Basi Vijana kuwa na misimamo mikali na kuwa na chuki na Serikali zao ndizo sababu kuu mbili za kuzuka kwa ogezeko la vijana kupotoshwa na kujiunga na makundi ya Kigaidi unaopelekea jinai za maangamizi na kupoteza amani ya watu wote bila kuangalia Imani za dini zao.
Itambulike kuwa, vitendo vya kigaidi havina mahusiano na dini ya kiislamu wala dini yeyote ile bali kuna baadhi ya vikundi vya watu ambao wanatumia mgongo wa dini ya hasa ya kiislamu kufanya vitendo vya kiarifu na uvunjifu wa amani, hivyo wakati mwengine hutumia mafundisho ya Quraan kupotosha vijana wengi duniani ili kuwahadaa na kupata wafuasi wapya wa kujiunga nao katika kutekeleza matakwa yao waliyokusudia.
Ugaidi ni janga kubwa duniani kote, ambapo umekuwa ukienea siku hadi siku kwa wanadamu ambao wamekosa fikra na utu ndani yake bila kujali Taifa wala dini yeyote hivyo yatupasa kuungana kutoa elimu na mafunzo sahihi hasa kwa watu ambao hawana elimu hii itasaidia kuepusha makundi haya ya kihalifu kuwalaghai wananchi kwa kisingizio cha kutaka kusimamisha dola ya kiislamu ulimwenguni.
Ni vyema watu kuondokana na kutokubaliana na dhana ya mafundisho ya dini ya kiislamu kutumiwa na kuhusishwa na vitendo vya kigaidi na kujaribu kufungamanisha dini hiyo na jinai wakati wanaofanya upotofu huo ni kwa makusudi na baadhi yao lengo lao wapate wafuasi wapya bila ya kujali kwamba wahusika hao wa jinai wanauchafua uislamu na wanaenda kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu.
Kuituhumu dini ya kislamu kuwa ni dini ya kigaidi, inachochea chuki kwa wale wasiyo kuwa na fikra hizo kujiunga na msimamo wa Imani ya itikadi kali na baadae kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi wakiwa na dhamira ya kuitetea dini yao. Moja ya malengo ya vikundi hivyo ni kutumia dini ya kiislamu kama propaganda ambapo dini zingine zitakuwa zinautuhumu uislamu na kuchochea chuki kwa waislamu safi na kuweza kujiunga na ugaidi.
Hivyo uwepo wa makundi ya kigaidi yanayojita makundi ya kiislamu kote duniani haimaanishi kuwa uislamu umewaamuru au kuwaelekeza kufanya jinai hizo, bali wanafanya vitendo hivyo kwa nia ovu na malengo yao binafsi kwani uislamu umesisitiza kuheshimu dini zote, kulinda uhai wa kila mmoja na kupendana.
Wito wangu ni vyema kila mmoja kuhakikisha kuwa amani na utulivu ni muhimu kwa jamii na Nchi kwa ujumla kwakuwa hata mafundisho ya dini zote yaemeletwa ili kufanya dunia iwe sehemu salama ya kuishi na sio mahala pa kuvujisha damu kwa watu wasio na hatia.
0 Comments