UISLAMU NI DINI YENYE MAADILI MEMA NA KUWATENDEA MEMA WASIO WAISLAMU
MWENYEZI Mungu (S.W) amemtuma Mtume wake Muhammad (S.A.W.) kwa ajili ya rehma kwa walimwengu wote, ambapo Mwenyezi Mungu (S.W) amesema "Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote" Surat Al - Anbiyaa, aya 107.
Uislam umewahimiza Waislam wawe na rehma na huruma kwa viumbe wote waliopo duniani, Mtume Muhammad (S.A.W) amesisitiza maana hiyo kwa kusema "Hakika Mwenyezi Mungu hawarehemu wasiowarehemu wanandamu".
Hivyo, Wanadamu wote wanatakiwa kuwa na huruma bila kujali itikadi ya dini zao, kabila wala rangi, ambapo moja wapo ya misingi ya tabia njema katika dini hiyo ni kuwaonea huruma wasio Waislamu na kuwatendea wema madhali hawawaudhi waislamu wala hawawafanyii uadui.
Kwani, huruma katika Uislamu ni jambo la viumbe wote, siyo kwa watu maalumu wala kwa baadhi ya Viumbe tu. Mtume Muhammad (S.A.W) amesema; "Kwa kweli Mwenyezi Mungu hamuhurumii ila aliye wahurumia wengine, Maswahaba wakasema; Ewe Mtume! Sote hivyo kwa maana tunawahurumia wengine. Mtume akasema, sikusudii mnavyofanya na wenzenu, bali na wanadamu wote".
Hivyo, alama ya kwanza ya ustahamilivu katika mfumo wa maadili mema ya kiislam ni kuwahurumia viumbe wote.
Mtume Muhammad (S.A.W) amesema kuwa aliadhibiwa mwanamke kwa ajili ya kumtesa Paka aliye mfungia ndani hakumpa chakula wala hakumuachia ajitafutie mwenyewe chakula, jambo hilo likasababisha aingie motoni. Katika hadithi hii tunajifunza jinsi huruma ilivyokuwa muhimu kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya kiislam.
Mtume alikuwa ni mfano bora wa huruma kwa viumbe wote hata wanyama, katika maelekezo kwa umma huu anasema (Hakika Allah ameagiza kufanya wema katika kila kitu hivyo hata mkichinja wanyama kwa ajili ya chakula wachinjeni vizuri) na katika hadihi nyengine anasema (mmoja wenu akimchinja mnyama anoe kisu chake vizuri na amlaze vizuri mnyama anayemchinja iliafanye jambo hilo kwa haraka).
0 Comments