BAADHI YA AYA ZA QURAAN ZINAZOTUMIKA KUUCHAFUA UISLAMU NA KUPOTOSHA WATU KUFANYA MATENDO MAOVU
Imeandikwa na SHEIKH JUMA SS
UISLAMU ni mtindo au mfumo wa maisha yote ya mwanadamu, mfumo au mtindo huo wa maisha unamuelekeza na kumuongoza mwanadamu katika kutenda mema hapa duniani ili awe na mwisho mwema kesho akhera.
Mafundisho ya kiislamu yameletwa na kufundishwa kupitia Quraan tukufu, sunna na hadithi za Mtume Mohammad (S.A.W). Hata hivyo kuna baadhi ya watu ambao hawautakii wema uislamu na wanachafua taswira ya dini kwa kutumia baadhi ya aya za Quraani katika kupotosha watu wengine kufanya matendo maovu kama vile harakati za ugaidi.
Aidha, baadhi ya aya ambao zilizotumika kufanya upotoshaji ni kama aya 214 Surat Bagara, Aya hii inaeleza kuwa "je mnadhani mtaingizwa peponi bila ya kujaribiwa kama walio kuwa kabla yenu? Walipatwa na dhiki na wakatikisika Sana hata na mtume na waumini pamoja naye wakasema: "lini nusura ya mwenyezi Mungu itakuja? Hakika nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu".
Lengo lao la kufundishwa aya hii ni kutiwa moyo kuwa wasirudi nyuma na mapambano ya kiharakati. Ila maana sahihi ya aya hiyo ni ilikuwa ni kuwaliwaza waumini wa dini ya kiislamu ambao walikuwa wakiteswa na makuraishi na kufanyiwa aina mbalimbali ya uonevu na udhalilishaji na kufikia wengine kukata tamaa, hivyo aya hii inawataka waumini wa dini ya kiislamu kuwa wavumilivu pindi wanapopatwa na matatizo na haikuletwa mahsusi kwa ajili ya vita. Kwakuwa aya hii inaelezea kuwa na uvumilivu washawishi wanaitumia aya hiyo katika muktadha wa kuwa wavumilivu na ujasiri wakiwa vitani.
Kutokana na mfano wa hapo juu inaonekana wazi jinsi gani maandiko haya matukufuanavyoweza kutumiwa vibaya na makundi ya wanaharakati wa kigaidi kuyafikia malengo yao. Hivyo ipo haja kwa wataalamu wa tafsiri kuwaelezea waumini malengo na makusudio sahihi ya hizi aya na jinsi ya kuzioanisha na mazingira ya sasa ili kuondoa upotoshaji unaoweza kutokea.
Aya ya 96 katika Surat al Nisai, aya hii imeeleza kuwa, "Wale wanaokaa nyumbani isipokuwa kwa wenye visingizio vilivyo halali hawawi sawa na wale wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao". "Mwenyezi Mungu amewanyanyua daraja wale wanaopigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao juu ya wanaobaki nyuma "kwa udhuru ulio sahihi" Mwenyezi Mungu amemuahidi kila mmoja ujira mzuri. Lengo la kufundishwa aya hii ni kuwashawishi vijana kwenda HIJRA kupigania dola la kiislamu.
Aya ya 4 Katika Surat Mohammed, Aya hii imeeleza kuwa, "Basi mnapokutana na makafiri katika vita, basi wapigeni shingo zao mpaka mzishinde kabisa, kisha zifungeni kwa nguvu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelitaka, yeye mwenyewe angeli waadhibu. Lakini yeye hufanya hivi ili kuwajaribu baadhi yenu kwa wengine. Na wale waliouawa kishahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, hatazibatilisha vitendo vyao". Lengo kufundishwa aya hii ni kuhalalisha vitendo vya mauwaji kwa wale wanaowaita makafiri.
Aya ya 191 katika Surat Al Baqara, Aya hii imeeleza kuwa, "waueni popote mnapowajia na muwatoe katika sehemu ambazo wamekutoeni. Kwa maana mateso ni mabaya zaidi kuliko kuua.
Wala msipigane nao katika Msikiti mtakatifu isipokuwa watakushambulieni humo. Wakifanya hivyo basi piganeni nao hayo ni malipo ya makafiri". Lengo la kufundishwa aya hii ni kulipa kisasi na mapigano kwa wanaowaita maadui zao.
Aya ya 193 katika Surat Baqara, Aya hii imeeleza kwamba, "piganeni nao wakikuudhini mpaka kusiwe na mateso na ibada yenu itakuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake . Wakiacha kuwatesa, basi usiwepo uadui ila kwa mwenye uvamizi". Lengo la aya hii ni kuhimiza uadui kwa wale wanaowaita makafiri.
Wito kwa wanazuoni wa dini ya kiislamu nchini, kusaidia kutoa mafundisho na tafsiri sahihi ya aya hizo ili kuzuia makundi ya vijana kuingia katika harakati za kigaidi na kuleta athari kwa Taifa na familia zao kwa ujumla.
0 Comments