TUMUOMBE MWENYEZI MUNGU ATUFIKISHE MWEZI WA RAMADHANI
Na Abdul A Rashad
As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakat!
Mwezi wa Ramadhani ni miongoni mwa miezi mitukufu na yenye fadhila kubwa katika Uislamu. Ni mwezi wa rehema, msamaha na kuokolewa na Moto wa Jahannam. Kwa sababu ya cheo chake kikubwa, Waumini wanahimizwa kumuomba Mwenyezi Mungu awape uhai, afya na tawfiq ya kuufikia mwezi huu ili wanufaike na baraka zake. Qur’ani Tukufu na Sunnah ya Mtume Muhammad (S.A.W.) zimeeleza wazi umuhimu wa Ramadhani na thamani ya dua.
Hakika Ramadhani ni Mwezi Uliobarikiwa, Mwenyezi Mungu anasema:
“Mwezi wa Ramadhani ni mwezi ulioteremshwa Qur’ani, uwe ni uongofu kwa watu na dalili zilizo wazi za uongofu na upambanuzi.”Suratul-Baqarah 2:185. Aya hii inaonesha kuwa Ramadhani ni mwezi wa uongofu na nuru, hivyo kuufikia ni neema kubwa inayopaswa kuombwa.
Kuomba kuufikia wakati wa kheri ni sunnah ya waumini, Mwenyezi Mungu anasema: “Na sema: Mola wangu! Niongezee elimu.”Suratu Taha 20:114. Aya hii inaonesha kuwa kuomba kuongezewa kheri na manufaa ya kiroho ni jambo linalopendwa. Vivyo hivyo, kumuomba Mwenyezi Mungu atuongezee uhai ili tufikie Ramadhani ni dua yenye msingi wa Kiislamu.
Mtume (S.A.W.) alitufundisha kuthamini uhai na wakati, Mtume Muhammad (S.A.W.) amesema: “Tumia vyema mambo matano kabla ya mambo matano: uhai wako kabla ya mauti yako…”Hadithi Hasan: Al-Haakim.Hadithi hii inatukumbusha kuwa kuufikia Ramadhani si jambo la uhakika; ni neema inayohitaji dua na maandalizi.
Ramadhani ni msimu wa rehema na msamaha. Mtume (S.A.W.) amesema: “Inapofika Ramadhani, milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa, na mashetani hufungwa.”Sahih Al-Bukhari na Sahih Muslim.
Kwa sababu ya fadhila hizi, Muumini wa kweli huomba: “Ewe Mwenyezi Mungu, tufikishe Ramadhani ili tunufaike na rehema zako.”
Thawabu ya kufunga ramadhani ni kubwa sana, Mtume Muhammad (S.A.W.) amesema: “Yeyote atakayefunga Ramadhani kwa imani na kutarajia thawabu, atasamehewa madhambi yake yaliyopita.”Sahih Al-Bukhari na Sahih Muslim.Hii inaonesha kuwa kuufikia Ramadhani ni fursa ya kufutwa madhambi, jambo linalostahili kuombwa kwa dhati.
Dua ni silaha ya muumini, Mwenyezi Mungu anasema: “Na Mola wenu amesema: Niombeni, Nitakujibuni.”Suratu Ghaafir 40:60. Kuomba kufikishwa Ramadhani ni dua iliyojaaunyenyekevu, matumaini, na hamu ya ibada.
Maswahaba walikuwa wakimuomba mwenyezi mungu awafikishe Ramadhani. Imepokelewa kuwa Maswahaba, walikuwa wakimuomba Mwenyezi Mungu miezi kabla ya Ramadhani awafikishe, na baada ya Ramadhani walimuomba akubali ibada zao. Hii inaonesha ufahamu wao wa thamani ya Ramadhani.
Ramadhani ni fursa isiyorudiwa, Mtume (S.A.W.) amesema: “Amepata hasara mtu aliyeifikia Ramadhani kisha akatoka bila kusamehewa.”Hadithi Sahihi: At-Tirmidhiy. Hadithi hii inatuhimiza kuutamani Ramadhani, kuomba kuufikia, na kujiandaa nao kwa ikhlasi.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W.), Ramadhani ni mwezi wa uongofu, mwezi wa msamaha na mwezi wa neema zisizopimika.
Hivyo, ni wajibu kwa kila Muumini kumuomba Mwenyezi Mungu awafikishe mwezi wa Ramadhani akiwa na uhai, afya na imani, ili autumie vizuri katika Swala, Saumu, Qur’ani na matendo mema.
1 Comments