UISLAMU UNAKATAZA VITENDO VIOVU, ASIYEFUATA ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU
Na Abdul A Rashad
As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakat! Uislamu ni dini ya haki, maadili na usafi wa maisha. Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta‘ala) aliuteremsha Uislamu ili kuongoza mwanadamu kutoka gizani kwenda kwenye nuru, kutoka katika upotofu kwenda kwenye uongofu, na kutoka kwenye maovu kwenda kwenye mema. Miongoni mwa misingi mikuu ya Uislamu ni kukataza vitendo viovu (maasi) na kuhimiza utiifu kwa Mwenyezi Mungu. Yeyote anayevunja mipaka ya Mwenyezi Mungu na kukaidi amri Zake, basi amejitwika juu yake adhabu kali, kwani Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Vitendo viovu ni kila jambo analolikataza Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (S.A.W). Hivi vinaweza kuwa Maovu ya kimaadili (uzinzi, uasherati, ushoga), Maovu ya kiitikadi (shirk, unafiki), Maovu ya kijamii (dhuluma, uonevu, rushwa), Maovu ya kifedha (riba, wizi, hadaa) na Maovu ya kitabia (uongo, husuda, fitina).
Uislamu haukatazi maovu kwa kubana uhuru wa mwanadamu, bali kwa kulinda heshima, maisha na Akhera ya mwanadamu.
Allah anakemea uchafu na maovu, Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu, ihsani na kuwapa jamaa, na anakataza uchafu, maovu na uadui.”(Surat An-Nahl: 90).
Aya hii ni msingi mkubwa wa maadili ya Kiislamu, ikionesha wazi kuwa Uislamu unasimama juu ya mema na kuupinga uovu.
Mwenyezi Mungu amesema: “Wala msikaribie uzinzi; hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa.” (Surat Al-Israa: 32). Aya hii haikatazi tu uzinzi, bali hata njia zinazopelekea uzinzi.
Maasi ya aina yeyote ile ikiwemo ugaidi huleta adhabu, Mwenyezi Mungu anasema: “Na yeyote anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na akavuka mipaka Yake, atamuingiza Motoni adumu humo, naye atapata adhabu ya fedheha.” (Surat An-Nisaa: 14). Aya hii inaweka wazi hatima ya asiyeifuata njia ya Allah.
Hadithi za Mtume (S.A.W) kuhusu maovu na adhabu, Mtume Muhammad (S.A.W) amesema: “Jihadharini na madhambi, kwani madhambi huangamiza.” (Imepokewa na Ahmad)
Pia dhambi hufanya moyo kuwa mweusi,Mtume (S.A.W) amesema: “Mja anapofanya dhambi, huwekwa nukta nyeusi moyoni mwake…” (Imepokewa na At-Tirmidhiy). Hii inaonyesha kuwa maasi huathiri imani na ucha-Mungu.
Mtume (S.A.W) ameongezea kwa kumesema: “Atakayeona uovu, aubadilishe kwa mkono wake; asipoweza, kwa ulimi wake; asipoweza, basi kwa moyo wake, na hiyo ni imani dhaifu.” (Imepokewa na Muslim)
Qur’ani imetaja mifano ya mataifa yaliyoadhibiwa kwa sababu ya maasi yao, kama Watu wa Nuhu (A.S)walizama kwa mafuriko, Watu wa Luti (A.S) waliangamizwa kwa maovu ya kimaadili, Watu wa ‘Aad na Thamud waliadhibiwa kwa ukaidi.
Mwenyezi Mungu anasema “Na kila mmoja tulimchukulia kwa dhambi yake.” (Surat Al-‘Ankabut: 40)
Allah ni Mkali wa Kuadhibu lakini ni Mwingi wa Rehema, Pamoja na onyo kali, Uislamu ni dini ya rehema. Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Mola wako ni Mkali wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Surat Al-A‘raaf: 167)
Hii inaonyesha mizani ya Uislamu: hofu na matumaini. Mtume (S.A.W) amesema: “Kama msingetenda dhambi, Mwenyezi Mungu angewaleta watu wengine watakaotenda dhambi kisha waombe msamaha, naye awasamehe.” (Imepokewa na Muslim)
Njia ya kujilinda na adhabu ya Allah ni Kutekeleza amri za Allah, Kujiepusha na makatazo, Kutubu toba ya kweli, Kushikamana na Swala na Qur’ani, Kuchagua marafiki wema na Kuamrisha mema na kukataza mabaya.
Uislamu umekuja kuondoa maovu na kuimarisha mema. Yeyote anayefuata njia ya Allah hupata heshima, amani na wokovu. Lakini asiyeifuata, akaendelea kufanya vitendo viovu bila kutubu, basi ajue kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu, na adhabu Yake ni ya haki. Ni wajibu wetu sote kurejea kwa Allah kabla haijafika siku ambayo majuto hayatatusaidia.
0 Comments