Miongoni mwa misingi mikuu ya Uislamu ni kusimamisha haki na uadilifu katika nyanja zote za maisha. Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta‘ala) ameharamisha dhuluma kwa aina zote, na ameifanya kuwa miongoni mwa madhambi makubwa yanayoangamiza mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Dhuluma inapohusishwa na mali, madhara yake huwa makubwa zaidi, kwani huathiri maisha, heshima na haki za watu.
Mali inayopatikana kwa dhuluma huonekana kuwa ni mafanikio kwa macho ya dunia, lakini mbele ya Mwenyezi Mungu ni hasara tupu, na mwisho wake ni majuto makubwa duniani, kaburini na Akhera.
Dhuluma katika mali ni kuchukua haki ya mtu bila ridhaa yake, iwe kwa wizi, rushwa, hadaa, riba, udanganyifu, au kutumia madaraka vibaya. Mwenyezi Mungu amekataza dhuluma kwa njia zote kwa sababu inavunja haki na huleta chuki katika jamii.
Mwenyezi Mungu (S.W.T) anasema: “Wala msiliane mali zenu kwa batili baina yenu, isipokuwa iwe biashara kwa ridhaa yenu.” (Surat An-Nisaa: 29). Aya hii inaonesha wazi kuwa mali inayopatikana kwa njia isiyo halali ni batili mbele ya Mwenyezi Mungu.
Aidha Mwenyezi Mungu anasema: “Na wala msile mali ya watu kwa dhuluma, mkapeleka kwa mahakimu ili mle sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, hali mnajua.” (Surat Al-Baqarah: 188). Aya hii inawakemea wale wanaotumia ujanja wa sheria au rushwa ili kupata mali isiyo yao.
Mtume Muhammad (S.A.W) alionya vikali juu ya kula mali ya watu kwa dhuluma. Imepokelewa kuwa amesema: “Atakayenyakua hata kipande cha ardhi kwa dhuluma, atavikwa shingoni mwake ardhi saba Siku ya Kiyama.” (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim). Hadithi hii inaonyesha adhabu kali inayomsubiri dhalimu Akhera.
Katika Hadithi nyingine Mtume (S.A.W) amesema: “Mwenyezi Mungu ni Mwema na hapokei isipokuwa kilicho chema.” (Imepokewa na Muslim)
Hii inaashiria kuwa ibada na dua za mtu anayekula mali ya haramu huwa hazikubaliki.
Mali ya dhuluma huleta madhara makubwa katika maisha ya mtu, yakiwemo Kukosa baraka hata kama mali ni nyingi, haitoi utulivu wala furaha,Migogoro na chukihuzaa uadui na kuvunja undugu, Kuangamia kwa jamii dhuluma ikipewa nafasi huangamiza taifa na Majuto makubwa hasa pale mauti yanapokaribia
Mwenyezi Mungu anasema: “Na usiwadhani Mwenyezi Mungu amezembea na yale wayatendayo madhalimu; bali anawaakhirisha mpaka siku ambayo macho yatakodoa.” (Surat Ibraahim: 42)
Mali halali ni chanzo cha baraka, Kinyume cha mali ya dhuluma, mali halali huleta baraka, utulivu wa moyo na kukubalika kwa dua. Mtume (S.A.W) aliwahimiza Waislamu kutafuta riziki kwa njia halali hata kama ni kidogo.
Amesema Mtume (S.A.W):
“Hakuna nyama iliyokua kwa haramu ila Moto unastahiki zaidi.” (Imepokewa na At-Tirmidhiy)
Ili kuiepuka mali ya dhuluma, Muislamu anatakiwa Kuogopa Mwenyezi Mungu katika kila muamala, Kurudisha haki alizochukua kwa dhuluma, Kutubu toba ya kweli kabla ya mauti na Kuridhika na kipato halali hata kama ni kidogo
Hakika mali ya dhuluma ni majuto, kwani haina baraka duniani na huleta adhabu Akhera. Mafanikio ya kweli kwa Muislamu si wingi wa mali, bali ni uadilifu, uhalali na ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Ni wajibu wetu kuishi kwa haki, kuheshimu mali za watu, na kutafuta riziki kwa njia halali ili tuokoke na majuto yasiyo na faida.
0 Comments