Siku ya Ijumaa ni siku tukufu na yenye cheo cha juu katika Uislamu. Mwenyezi Mungu ameifanya iwe ni siku ya ibada ya pamoja, dhikri, dua na kusamehewa madhambi. Qur’ani Tukufu na Sunnah ya Mtume Muhammad (S.A.W.) zimeeleza wazi fadhila na ubora wa siku hii kuliko siku nyingine zote.
Ijumaa ni siku iliyotajwa moja kwa moja ndani ya qur’ani, Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Inapoitwa Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu na muache biashara.”Suratul-Jumu‘ah 62:9
Aya hii inaonesha Ubora wa Swala ya Ijumaa, Ulazima wa kuipa kipaumbele ibada kuliko shughuli za dunia, Ijumaa ni siku ya dhikri na kukutana kwa Waumini.
Ijumaa ni siku bora zaidi katika wiki, Mtume Muhammad (S.A.W.) amesema: “Siku bora zaidi iliyochomoza jua ni siku ya Ijumaa; humo aliumbwa Adam, humo aliingizwa Peponi, na humo alitolewa Peponi.”Sahih Muslim. Hadithi hii inaonesha kuwa Ijumaa ni siku yenye historia kubwa ya mwanzo wa maisha ya mwanadamu.
Ijumaa ni siku ya msamaha wa madhambi, Mtume (S.A.W.) amesema: “Swala tano, Ijumaa hadi Ijumaa, na Ramadhani hadi Ramadhani ni kafara ya madhambi yaliyo kati yao, iwapo madhambi makubwa yataepukwa.”Sahih Muslim. Hii ni bishara njema kwa Waumini kuwa Ijumaa ni nafasi ya kujisafisha kiroho.
Ijumaa ni siku ya kujibu dua, Mtume Muhammad (S.A.W.) amesema: “Katika siku ya Ijumaa kuna saa ambayo Muislamu akiswali na kumuomba Mwenyezi Mungu kitu chochote chema, Atampa.”Sahih Al-Bukhari na Muslim.
Hivyo, Waumini wanahimizwa Kuongeza dua, Dhikri, Kusoma Qur’ani, hasa Suratul-Kahf.
Fadhila ya kusoma qur’ani siku ya ijumaa, Mtume (S.A.W.) amesema: “Atakayesoma Suratul-Kahf siku ya Ijumaa, atapatiwa nuru baina ya Ijumaa mbili.”Hadithi Hasan: Al-Haakim. Hii ni ishara ya baraka na ulinzi wa Mwenyezi Mungu.
Ijumaa ni Siku ya Swala ya Jamaa na Umoja, Mwenyezi Mungu anasema:
“Hakika Waumini ni ndugu.” Suratul-Hujuraat 49:10 Swala ya Ijumaa hukusanya Waumini pamoja huimarisha umoja, hueneza nasaha, hujenga mshikamano wa Umma.
Adabu na sunnah za siku ya ijumaa, Mtume (S.A.W.) amesema: “Anayejitwaharisha vizuri siku ya Ijumaa, akaoga, akapaka manukato, akaswali alichoandikiwa, kisha akanyamaza wakati wa khutba, atasamehewa madhambi yake yaliyo kati ya Ijumaa mbili.”Sahih Al-Bukhari. Hii inaonesha umuhimu wa Usafi, Nidhamu, Kusikiliza khutba kwa makini.
Ijumaa ni sikukuu ya waumini, Mtume Muhammad (S.A.W.) alisema: “Hakika hii ni siku ya sikukuu ambayo Mwenyezi Mungu Amewapa Waislamu.”Ibn Majah (Hadithi Hasan). Kwa maana hii, Ijumaa ni Eid ya kila wiki kwa Waumini.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W.), siku ya Ijumaa ni siku bora kuliko zote, ni siku ya ibada, dua na msamaha, ni siku ya umoja wa Waumini na ni fursa ya kumkaribia Mwenyezi Mungu.
Hivyo, ni wajibu kwa kila Muislamu kuiheshimu, kuitukuza na kuitumia Ijumaa kwa ibada na matendo mema, ili apate radhi za Mwenyezi Mungu na kufuzu Pepo.
0 Comments