As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakatuh! Uislamu ni dini ya haya (staha), heshima na ulinzi wa maadili ya jamii. Mavazi ya mwanamke Muislamu ni sehemu ya mfumo huu wa ulinzi. Katika muktadha huu, Niqāb (kufunika uso) imezungumziwa na wanazuoni kama njia mojawapo ya juu ya staha, hasa katika mazingira yenye fitna. Makala hii inalenga kueleza hekma na manufaa ya Niqāb kwa mujibu wa Qur’ani na Sunnah sahihi.
Mwenyezi Mungu anasema, lengo kuu la mavazi ya kiislamu na staha na kujitambua; “Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, wajisitiri tupu zao, wala wasidhihirishe uzuri wao…”Suratun-Nuur 24:31.
Aya hii inaweka kanuni ya msingi: kujisitiri na kulinda heshima. Niqāb huja kama hatua ya ziada ya tahadhari katika utekelezaji wa kanuni hii.
Niqāb na ulinzi dhidi ya dhara na fitna, Mwenyezi Mungu anasema: “Ewe Nabii! Waambie wake zako na binti zako na wanawake wa Waumini wajiteremshe jilbabu zao. Hiyo ni bora zaidi ili watambuliwe na wasidhuriwe.”Suratul-Ahzaab 33:59.
Hekma ya Aya ni Lengo ni ulinzi na heshima, Kuzuia kudhuriwa, kutamaniwa au kunyanyaswa, Niqāb kwa baadhi ya wanazuoni huingia katika njia ya juu zaidi ya utekelezaji wa amri hii, hasa panapokuwa na fitna.
Mtume (S.A.W.) alihimiza haya (Staha) amesema: “Haya ni sehemu ya imani.”Sahih Al-Bukhari na Sahih Muslim. Niqāb ni taswira ya kivitendo ya haya, kwa mwanamke anayechagua daraja la juu la staha.
Tukiangalia mfano wa wanawake wa Maswahaba, Bi ‘Aishah (R.A.) amesema kuhusu wanawake wa Answar: “Wanawake wa Answar walipo teremshiwa aya ya hijab, walichana mashuka yao na wakajisitiri nayo.”Sahih Al-Bukhari.
Hii inaonesha haraka ya utiifu na kuelekea kwenye kiwango cha juu cha staha, ambacho kwa baadhi yao kilihusisha pia kufunika nyuso katika mazingira ya fitna.
Niqāb pia kama kinga ya kimaadili katika jamii, Mwenyezi Mungu anasema: “Na msikaribie zinaa; hakika ni uchafu na ni njia mbaya.” Suratul-Israa 17:32
Uislamu hauzuii zinaa tu, bali unazuia njia zinazoelekea kwake. Niqāb: hupunguza vishawishi, hulinda heshima ya mwanamke na kusaidia jamii kuwa na nidhamu ya kimaadili.
Mtume (S.A.W.) na ulinzi wa heshima ya Mwanamke amesema: “Dunia ni mapambo, na pambo bora zaidi la dunia ni mwanamke mwema.”Sahih Muslim. Uwanamke mwema hujitambulisha kwa imani, tabia na staha, si kwa kudhihirisha uzuri wake. Niqāb humsaidia mwanamke kutambulika kwa uchaMungu, si kwa sura.
Tofauti za kifiqhi na hekima ya uchaguzi ni muhimu kufahamu kuwa na Wanazuoni wametofautiana kuhusu hukumu ya Niqāb (wajibu au sunnah/mubah kulingana na mazingira), Lakini wote wanakubaliana kuwa Niqāb ni njia ya staha ya juu, hasa panapokuwa na fitna. Uislamu hauwalazimishi wanawake kwa ukatili, bali huwainua kwa heshima na ulinzi.
Niqāb ni ibada inapofanywa kwa ikhlasi, Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Hakika Swala yangu, ibada zangu, maisha yangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.”Suratul-An‘aam 6:162.
Mwanamke anapovaa Niqāb kwa nia ya kumridhisha Mwenyezi Mungu, basi hugeuza vazi kuwa ibada, hupata thawabu na hupanda daraja la uchaMungu.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi, ni wazi kuwa Uislamu unahimiza staha, haya na ulinzi wa heshima pia Niqāb ni njia mojawapo ya juu ya kutekeleza misingi hiyo na chaguo lenye hekma ya kinga ya maadili, heshima na amani ya nafsi. Hivyo Mwanamke anayechagua Niqāb kwa ikhlasi anafuata njia ya utiifu na uchaMungu.
Hivyo, Niqāb si ukandamizaji, bali kwa anayechagua, ni heshima, ulinzi na ibada mbele ya Mwenyezi Mungu.
0 Comments