As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakatuh! Kuna dhana potofu inayosambazwa kwamba Uislamu unaruhusu au kuhalalisha kumpiga mwanamke. Dhana hii mara nyingi hutokana na kutoelewa Qur’ani kwa muktadha wake sahihi, kupuuza Sunnah ya Mtume Muhammad (S.A.W.), na kutafsiri aya kwa misingi ya hisia au mila badala ya elimu. Makala hii leo inalenga kuweka wazi msimamo wa Uislamu kwa kutumia Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W).
Kanuni ya msingi kwenye maisha ya ndoa yajengwe kwa wema na huruma. Mwenyezi Mungu anasema: “Na katika ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao, na Akaweka baina yenu mapenzi na rehema.”Suratur-Ruum 30:21
Aya hii inaweka msingi kuwa ndoa katika Uislamu inajengwa juu ya mapenzi, huruma na utulivu, si vurugu wala ukatili.
Katika Qur’ani Tukufu aya inayopotoshwa zaidi (Suratun-Nisaa 4:34). Mwenyezi Mungu anasema: “Na wale ambao mnahofia uasi wao, waonyeni, na waacheni peke yao vitandani, na (kama njia ya mwisho kabisa) waá¸ribÅ«hunna…”Suratun-Nisaa 4:34
Ufafanuzi sahihi wa kielimu, Aya hii haikuja kuhalalisha kumpiga mwanamke, bali kuweka mfumo wa kutatua migogoro ya ndoa hatua kwa hatua. Mfano sahihi Neno “waá¸ribÅ«hunna” katika lugha ya Kiarabu lina maana nyingi, zikiwemo kutenganisha, kuachana, au ishara ya nidhamu isiyo ya madhara.
Pia, wanazuoni wakubwa (kama IBN ABBAS) wamesema: Ikiwa itafikiwa hatua hii, basi ni kwa ishara isiyo na maumivu, isiyo ya kudhalilisha, na isiyo ya kuumiza.
Mtume Muhammad (S.A.W.) hakuwahi kumpiga mwanamke, Bi Aisha (R.A.) amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwahi kumpiga mwanamke wala mtumishi wake, wala hakuwahi kupiga chochote kwa mkono wake.”Sahih Muslim
Hii ni tafsiri ya vitendo (Sunnah Amaliyya) inayoonesha wazi kuwa Mtume hakutumia aya hiyo kama ruhusa ya kupiga.
Mtume (S.A.W.) alikataza kupiga wanawake, Mtume Muhammad (S.A.W.) alisema: “Msipige wake wa Mwenyezi Mungu.”Sunan Abu Dawud (Hadithi Sahihi)
Na pia alisema: “Je, mmoja wenu anampiga mkewe kama anavyompiga mtumwa, halafu jioni anamkumbatia?”Sahih Al-Bukhari na Muslim. Haya ni maneno ya wazi yanayokemea vikali vitendo vya vurugu ndani ya ndoa.
Bora zaidi kati ya waumini ni Mwenye tabia njema kwa mkewe. Mtume (S.A.W.) amesema: “Mbora wenu ni yule aliye mbora kwa watu wa nyumbani kwake, na mimi ni mbora zaidi kwenu kwa watu wa nyumbani kwangu.”Hadithi Sahihi: At-Tirmidhiy. Hivyo, kumpiga mwanamke ni kinyume na ubora wa imani.
Qur’ani inaharamisha dhuluma na uonevu, Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu hapendi madhalimu.”Suratu Aali ‘Imraan 3:57
Na pia: “Msidhulumiane.”Suratul-Baqarah 2:279. Kupiga mwanamke ni dhuluma ya wazi, na haiwezi kuhalalishwa kwa jina la dini.
Mwenyezi Mungu anasema: “Waisheni nao kwa wema.”Suratun-Nisaa 4:19. Na pale panapozidi ugumu, Qur’ani inaelekeza: “Kama mkihofia mgawanyiko kati yao, teule mjumbe kutoka kwa jamaa zake na mjumbe kutoka kwa jamaa zake…”Suratun-Nisaa 4:35. Hakuna sehemu Qur’ani inayohimiza vurugu kama suluhisho la kudumu.
Uislamu unalinda heshima ya mwanamke. Mtume (S.A.W.) alisema katika Khutba ya kuaga: “Waogopeni Mwenyezi Mungu katika (kuwahudumia) wanawake, hakika mmewachukua kwa amana ya Mwenyezi Mungu.”Sahih Muslim. Mwanamke katika Uislamu ni amana, si mali ya kupigwa.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na Hadithi sahihi za Mtume Muhammad (S.A.W.), ni wazi kwamba: Uislamu hauhalalishi kumpiga mwanamke, Mtume (S.A.W.) hakuwahi kufanya wala kuhimiza vitendo hivyo, Aya ya Suratun-Nisaa 4:34 imewekewa mipaka, muktadha, na tafsiri sahihi, Vurugu dhidi ya wanawake ni kinyume na maadili ya Kiislamu, rehema na uadilifu.
Hivyo, anayempiga mwanamke kwa jina la Uislamu amepotosha Qur’ani na Sunnah, na anawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu na jamii.
0 Comments