THAWABU ANAZOPATA MUUMINI ANAPOTEMBELEA WAGONJWA SIKU YA IJUMAA
Na Amina A. Juma
As-salamu alaykum wa raḥmatullahi wa barakatuh! Uislamu ni dini ya huruma, mshikamano na kujali hali za wengine. Miongoni mwa matendo mema yenye nafasi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuwatembelea wagonjwa. Kitendo hiki huonyesha upendo, huruma na udugu wa Kiislamu. Siku ya Ijumaa, ambayo ni siku tukufu kwa Waislamu, ibada na matendo mema hupewa uzito wa pekee. Hivyo, kumtembelea mgonjwa siku ya Ijumaa huunganisha fadhila ya siku tukufu na fadhila ya kitendo cha huruma.
Kutembelea Wagonjwa ni sehemu ya ihsani, Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu huamrisha uadilifu na ihsani.”Suratun-Nahl 16:90. Ihsani inajumuisha kuwajali wenye shida, wakiwemo wagonjwa. Kumtembelea mgonjwa ni utekelezaji wa moja kwa moja wa amri hii ya Qur’ani. Pia Mtume Muhammad (S.A.W.) alifundisha kwa vitendo ihsani hii kwa kuwajali wagonjwa na kuwatembelea mara kwa mara.
Waumini wote katika dini hii ni Ndugu, Hivyo Kusaidiana ni Wajibu. Qur’ani inasema: “Hakika Waumini ni ndugu.”Suratul Hujuraat 49:10. Udugu huu unawajibisha Waumini kujaliana, kufarijiana na kusaidiana wakati wa maradhi na dhiki.
Mtume (S.A.W.) amesema: “Hakuna Muislamu anayemtembelea Muislamu mwenzake asubuhi ila Malaika elfu sabini humwombea rehema mpaka jioni; na akimtembelea jioni, humwombea rehema mpaka asubuhi, na atapata bustani katika Pepo.”Hadithi Sahihi: Imepokewa na At-Tirmidhiy
Mwenyezi mungu anapenda wafanyao mema, Mwenyezi Mungu anasema:
“Na fanyeni mema; hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.”Suratul Baqarah 2:195. Kutembelea wagonjwa ni miongoni mwa matendo mema yanayomletea Muumini mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Siku ya Ijumaa ni siku ya ibada na kumbukumbu ya Mwenyezi Mungu, Qur’ani inaitukuza siku ya Ijumaa: “Enyi mlioamini! Inapoitwa Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu.”Suratul Jumu‘ah 62:9. Kufanya matendo mema siku hii huongeza ujira kwa sababu ya heshima ya siku yenyewe.
Mtume (S.A.W.) akasema: “Siku bora zaidi iliyochomoza jua ni siku ya Ijumaa.”Sahih Muslim. Hivyo, kufanya amali kama kutembelea wagonjwa siku hii huongeza fadhila na thawabu.
Ndugu yangu mwislamu tamua kuwa kutembelea wagonjwa ni dalili ya rehema. Mwenyezi Mungu anajitambulisha kuwa Mwingi wa rehema: “Na rehema Yangu imeenea kila kitu.”Suratul A‘raaf 7:156. Muumini anapowaonea wagonjwa huruma, hujiweka karibu na rehema za Mwenyezi Mungu.
Qur’ani inasema: “Kwa hakika katika kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndipo nyoyo hupata utulivu.”Suratur-Ra‘d 13:28. Muumini anapomtembelea mgonjwa kwa maneno ya matumaini na dua, humsaidia kupata utulivu wa moyo.
Kusaidia wenye dhiki hasa siku ya Ijumaa ni njia ya thawabu kubwa
Mwenyezi Mungu anasema: “Na anayefanya wema uzito wa chembe atauona.”Suratuz-Zalzalah 99:7. Hakuna wema unaopotea mbele ya Mwenyezi Mungu, hata ule wa kumtembelea mgonjwa kwa muda mfupi.
Qur’ani inawahimiza Waumini kushikamana: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote kwa pamoja.”Suratu Aal ‘Imraan 3:103. Kutembeleana huimarisha mshikamano, upendo na amani katika jamii ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, kumtembelea mgonjwa ni amali tukufu na yenye thawabu kubwa, na inapofanywa siku ya Ijumaa, ujira wake huongezeka kwa heshima ya siku hiyo. Kitendo hiki hutekeleza amri ya ihsani, huimarisha udugu wa Kiislamu, huleta rehema na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na humpatia Muumini thawabu zisizopimika.
Ni wajibu wa kila Muislamu kutumia siku ya Ijumaa sio kwa Swala pekee, bali pia kwa matendo ya huruma kama kuwatembelea wagonjwa, ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu duniani na Akhera.
1 Comments