KATIKA Makala hii, leo tutaangalia kwa namna gani suala zima la kudumisha amani na utuluvu, limepewa kipaumbele kwa mujibu wa mafunzo sahihi ya dini ya kiislam, hali hii ni tofauti dini hiyo inavyoonekana kutokana na vitendo vya baadhi ya watu wachache ambao wanachafua taswira yake nzuri na muhimu katika ustawi wa Jamii. Uislam ni dini ya amani na utulivu inayopinga vitendo vyote vinavyopelekea kuvunjika kwa amani, neno “ISLAAM” linatokana na neno la kiarabu “SILM” ambalo linamaanisha amani, katika mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W) Muislam halisi ameelezwa kuwa ni mtu ambaye hasababishi madhara kwa jamii yake kupitia maneno yake ama vitendo vyake. Ili kusisitiza umuhimu wa amani na utulivu katika maisha ya jamii, uislam umehimiza kuishi kwa amani katika jamii inayoundwa na wafuasi wa dini tofauti, katika Qur.an Sura ya 60 Aya ya 10 Mwenyezimungu (S.W) anasema “hakuzuieni Allah kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawajakupigeni vita katika dini yenu na hawajakutoeni kwenye majumba yenu, kwa hakika Allah anawapenda wenye kufanya uadilifu”. Kwa upande wake Mtume Muhammad (S.A.W) amekataza kumuua asiyekuwa muislam anayeishi kwa amani na Waislam, pale aliposema (atakaemuuwa asiye kuwa muislam anayeishi na waislam kwa amani basi hatoinusa harufu ya pepo na hakika harufu ya pepo inapatikana tokea umbali wa mwendo wa miaka arobaini) hadithi hiyo imepokelewa na Imam Bukhari, mafundisho haya ya Mtume yanaelekeza kuwa uislamu unapinga mauaji ya wasiokuwa na hatia hata kama sio waumini wa dini hiyo. Uislam umeenda mbali zaidi katika kupinga mauaji kwa kukataza mtu kujiua mwenyewe pale kiongozi mkuu Mtume Muhammad (S.A.W) aliposema “mwenye kujiuwa kwa chuma ataadhibiwa kwa chuma hicho akiwa ndani ya moto wa Jahannam” maana ya mafunzo haya ni kuwa kama ilivyokatazwa kuua watu wengine bila hatia imekatazwa pia mtu kukatisha maisha yake kwa kujiuwa yeye mwenyewe. Hivyo ni wajibu kwa kila Muislam kuwa mjumbe wa amani popote alipo na kutoichafua picha nzuri ya uislam iliyojengwa na mtume Muhammad (S.A.W), Maswahaba na watu wema waliopita ambao waliwavutia watu kuingia katika uislam kwa kuvutiwa na mafunzo ya amani kutoka kwa waislam. Aidha, baadhi ya mifano hai ya kulinda amani kutoka kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ni kama tukio la kukombolewa mji wa Makkah lililotokea tarehe 08 Mwezi wa Ramadhan mwaka wa 08 Hijriya sawa na tarehe 10 Januari Mwaka 630, viongozi wa kabila la Quraish walikuja mbele ya Mtume wanatetemeka kwa kuwa walimtesa na kumfanyia madhila ya kila namna, mtume aliwauliza “mnadhani nitawafanyaje leo hii?” wakiwa katika hali ya hofu walijibu “matarajio yetu utatufanyia wema kwani wewe ni ndugu mwema”. Mtume akawaambia nendeni nyote mpo huru. Hili ni somo tosha la kupenda amani, kwani Mtume aliwashinda maadui waliomtesa miaka ya nyuma na alikuwa na uwezo wa kuwafanya chochote atakacho lakini yeye aliamua kuawaachia huru. Mfano wa pili, Mtume Muhammad (s.a.w) alivyoingia Madina na kuwakuta Mayahudi wakiishi na jamii ya kiislam katika mji huo, ili kuhakikisha jamii hiyo inaishi kwa Amani na utulivu Mtume aliandika Mkataba wa amani na Mayahudi waliokuwa wanaishi katika Mji huo. Kipengele kikuu katika mkataba huo kilikuwa, kuishi kwa utulivu baina ya jamii zote za mji wa Madina wakati wa amani na kuutetea mji huo kwa pamoja pindi ukishambuliwa na adui, Mtume aliutekeleza na kuuheshimu mkataba huo mpaka mayahudi walivyo uvunja mkataba husika. Mfano mwingine, Mtume alipohamia Madina alikuta Makabila Makuu ya mji huo Awsi na Khazraji yakiwa katika hali ya kutoelewana akasuluhisha ugomvi huo na kuwafanya waishi wakiwa ndugu wanaopendana tukio hilo limeelezwa ndani ya kitabu kitukufu cha Qu.ran Sura ya 3 Aya ya 103. Hivyo, kutokana na mifano hii ni wazi kuwa mtu katili, muuwaji awezi kujinasibisha kuwa yeye ni muislam bora ama mfuasi wa mtume Muhammad (S.A.W) kwani mafundisho yake yamehimiza Amani na kupinga aina zote za uhalifu na ukatili, ni wajibu kwa kila Muislam kumuiga Mtume katika tabia yake ya kupenda amani. Nchini Tanzania tunaishi pamoja Jamii ya wafuasi wa dini mbali mbali sote tunakusanywa na jina moja la Watanzania,hivyo tunawajibu wa kuishi kwa Amani, na utulivu baina yetu na kuyafanyia kazi mafunzo haya mazuri ya Mtume yanayofundisha umuhimu wa kudimisha Amani na utulivu katika jamii.