UISLAMU NI DINI NYEPESI INAYOHIMIZA MSIMAMO WA KATI

Miongoni mwa misingi ya mafundisho ya dini ya kiislamu, ni pamoja na masuala ya ibada na mambo ya kijamii (muamalaat) ni kufanya mambo kwa wepesi na kuondoa uzito. Katika Qur’an sura ya pili aya ya (185) Allah (S.W) anasema “Allah anawatakieni wepesi na hakutakieni uzito”, sura ya nne aya 28 Allah anasema “Allah anawatakieni wepesi na binadamu ameumbwa dhaifu” Mama wa waumini Bibi Aisha anasema “Mtume akihiyarishwa kati ya vitu viwili huteuwa chepesi”. Katika vitabu vya sheria ya Kiislamu (FIQH), Kuna mifano kadha wa kadha inayowatakia wepesi waislamu. “Muumini wa dini ya kiislamu anapokuwa safarini anaruhusiwa kupunguza swala ya rakaa nne na kuswali rakaa mbili”, Anaruhusiwa kutanguliza swala ya alasiri na kuiswali kipindi cha adhuhuri, swala ya insha kuiswali kipindi cha magharibi na kufanya kinyume chake kwa maana adhuhuri kuiswali al.asr na Magharibi kuiswali kipindi cha insha, Kuhusu ibada ya funga ambayo ni moja ya nguzo za uislamu, msafiri na mgonjwa wameruhusiwa kuacha kufunga na kulipa idadi ya siku walizofungulia katika siku za mbele baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa ramadhan, hii inaonesha kwa jinsi gani dini hii inawahurumia wafuasi wake hata linapokuja suala la ibada. Mfano mwengine unaonesha uwepesi katika sheria za kiislamu ni swala zima la kuchukua udhu ama kujitwaharisha ili kutekeleza ibada, kimsingi tendo la kujitwaharisha linafanywa kwa maji, hata hivyo ikitokea maji hakuna au muumini hawezi kutumia maji kwa sababu zilizothibitishwa na daktari ipo ruhusa ya kutumia mchanga (kutaymmam) na kufanya ibada pasipo kutumia maji ambayo ndiyo msingi wa kujitwaharisha. Mafundisho ya uislamu yameweka wazi kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) alichagua jambo jepesi akishauriwa kuhusu mambo mawili ya kufanya ili kuwawepesishia wafuasi wake matendo ya ibada, Mathalan alikataza maimamu kurefusha ibada ya swala na kuwataka watoaji hotuba kufupisha hotuba za Ijumaa. Moja ya mifano ya wazi katika maisha ya Mtukufu wa daraja yanayoonesha namna dini ya uislamu ilivyo nyepesi ni tukio la Mtume Muhammad (S.A.W) alipomkuta mtu anatembea katika Hijja akiwa amechoka alipomuuliza akajibu alikweka nadhiri ya kutekeleza ibada hio akiwa anatembea kwa miguu ndipo mtume akamuamrisha apande mnyama na amalizie ibada ya Hijja akiwa amepanda. Katika suala la kuweka wakfu mali za muumin ili zitumike baada yake kwenye maswala ya kijamii kwa lengo la kupata ujira kutoka kwa Allah uislamu umeweka kiwango cha mwisho cha kutoa Waqfu kuwa ni moja ya tatu ya mali ama theluthi moja kwa lengo la kubakisha theluthi mbili zibakie kwa warithi, kwa lengo la kuwasaidia familia ya marehemu. Maelezo hayo yapo katika kisa cha Mtume (SAW) alipo mtembelea mfuasi wake (swahaba) anaetambulika kwa jina la SAAD, ambaye alikuwa mgonjwa mahututi, mfuasi huyo aliusia mali yake yote itolewe kwa ajili ya Allah (S.W) Mtume akamuelekeza kuwa atoe theluthi ya mali na kwamba kiasi hicho kinatosha na kwamba bora awaache watoto wake wakiwa wana hali njema ya maisha kuliko kuwaacha masikini wanawaomba watu. Katika maisha ya ndoa uislamu umeruhusu kuachana inapotokea maisha ya watu wawili pamoja yameshindikana hii ni kwa lengo la kuepusha mauaji, kupigana au kufanyiana uadui wowote, na umemruhusu mwanamke kuivunja ndoa anapokosa mambo muhimu katika ndoa hiyo kwa lengo la kumpa kila mtu haki ya kusheherekea maishja yake hapa duniani. Hivyo, tukiangalia mifano yote iliyo elezwa hapo juu tunabaini kuwa waumini wanaoweka ugumu katika dini na kuishi maisha ya tabu wakifikiri kuwa huo ndio mwenendo sahihi wa uislamu wanapotosha mafunzo ya dini ya kiislamu, kwani huo sio msimamo sahihi wa uislamu bali uislamu ni dini nyepesi na inapenda uwepesi katika mafunzo yake na uislamu siyo dini ya ukatili na roho ngumu. Ni wito wangu kwa waumini wote wa dini ya kiislamu waoneshe uwepesi wa mafunzo ya dini ya kiislamu katika maisha yao ya kila siku ikiwemo kutofanya vitendo vya kujiwekea uzito mathalan, kuna baadhi ya waislamu wanaharamisha na kuviita ni ukafiri vitu halali kama kuangalia runinga kusikiliza Redio na mambo mengine ambayo kwa mujibu wa uislamu ni halali.